Zenj FM

SMZ yaahidi kuimarisha huduma kwa wagonjwa wa kisukari

14 November 2025, 8:33 pm

Mkurugenzi wa Kinga na Elimu ya Afya, Dk. Salim Slim, akizungumza wakati akifungua kongamano maalum la wadau wa ugonjwa wa kisukari lililoandaliwa na Jumuiya ya Kisukari Zanzibar (DAZ).

Na Mwandishi wetu

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema itaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha ustawi wa watu wanaoishi na changamoto za ugonjwa wa kisukari unaimarika.

Mkurugenzi wa Kinga na Elimu ya Afya, Dk. Salim Slim, amesema hayo wakati akifungua kongamano maalum la wadau wa ugonjwa wa kisukari lililoandaliwa na Jumuiya ya Kisukari Zanzibar (DAZ), lililofanyika katika Skuli ya Sekondari Tumekuja, Wilaya ya Mjini, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kisukari Duniani.

Amesema Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuwekeza katika maradhi yasiyoambukiza ili kuhakikisha kila mwenye changamoto ya ugonjwa huo anapata huduma stahiki kwa wakati.

Aidha, amesema Serikali inatambua changamoto zinazowakabili wagonjwa wa kisukari na itaendelea kuchukua mbinu mbalimbali kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Akisoma risala ya kongamano hilo, Naibu Katibu wa Jumuiya ya Kisukari Zanzibar (DAZ), Rukia Mgongo, amesema takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya watu milioni 500 duniani wanaishi na ugonjwa wa kisukari, na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka ifikapo mwaka 2030, ikiwemo Tanzania.

Ameeleza kuwa idadi ya watu wanaoishi na kisukari inaongezeka mwaka hadi mwaka kutokana na mtindo wa maisha usiozingatia lishe bora, ulaji wa vyakula visivyo na uwiano, ukosefu wa mazoezi, na ongezeko la uzito kupita kiasi.

Kwa upande wa Zanzibar, amesema ripoti ya Wizara ya Afya ya mwaka 2023 inaonesha kuwa kati ya wagonjwa 56,983 waliolazwa, 1,818 sawa na asilimia 32, ni wagonjwa wa kisukari, na kati yao 29, sawa na asilimia 3.1, walifariki dunia.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa DAZ, Haji Abdalla Ameir, ameitaka jamii kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara na kufuata ushauri wa wataalamu ili kupunguza athari za ugonjwa huo.

Ameongeza kuwa ongezeko la wataalamu wa dawa za asili bila uangalizi, pamoja na ulaji wa vyakula visivyo na ubora wa lishe, kunachangia kuibuka kwa maradhi mengine kama vile ya figo na kuongeza idadi ya wagonjwa wapya wa kisukari.

Akizungumzia upande wa saikolojia, Mwenyekiti huyo amesema wagonjwa wengi hukosa msaada wa kisaikolojia, jambo linalowapa wasiwasi na kusababishwa na kuongezeka kwa athari za ugonjwa huo.