Zenj FM
Zenj FM
8 November 2025, 9:32 pm

Na Mary Julius.
Katika kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora, walimu wametakiwa kutumia mitaala mipya ya elimu ufuili kuwawezesha wanafunzi kupata maarifa na ujuzi utakaowaandaa kwa maisha ya baadae.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Magharibi “A”, Afisa Elimu Ufuatiliaji Utendaji Kazi wilaya ya Magharib A Issa Kefa Barthazar, katika hafla ya kuwazawadia wahitimu wa kidato cha nne, elimu ya msingi na elimu ya maandalizi wa skuli ya Herrnhuter Academy iliyofanyika huko Mwera, amesema mtaala mpya wa elimu unalenga kujenga uwezo wa wanafunzi katika vitendo zaidi, ili waweze kujitegemea na kujiendeleza kielimu na kimaisha.
Ameongeza kuwa ili kufikia malengo ya kuwa na wataalamu nchini, ni muhimu walimu na wazazi kushirikiana kuhakikisha wanafunzi wanasoma kwa bidii.
Aidha, amewataka wanafunzi wa kidato cha nne kutumia muda huu wa maandalizi kujisomea kwa makini, akisisitiza kuwa katika wilaya hiyo hawataki kuona matokeo ya Division Four wala Division Zero.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Skuli hiyo Geofrey Mkumbwa, amesema kuwa hatua ya serikali kuendelea kuboresha miundombinu ya elimu inapaswa kuungwa mkono, na kuwataka wanafunzi kujituma zaidi kwa manufaa yao binafsi na maendeleo ya taifa.
Nae Mmoja wa wahitimu wa darasa la saba, Catherine Evarist Tadei, ambaye aliongoza kwa ufaulu na nidhamu, amewasihi wanafunzi wenzake kusoma kwa bidii na kuwa na nidhamu ili kufanikiwa katika masomo na maisha.
Skuli ya Herrnhuter Academy, inayomilikiwa na Kanisa la Moraviana, ilianzishwa mwaka 2013 ikiwa na wanafunzi watatu pekee, na hadi sasa imefikisha wanafunzi 719. Skuli hiyo inatoa ufadhili kwa wanafunzi 37, baadhi yao wakiwa ni miongoni mwa wahitimu wa mwaka huu ambapo wanafunzi 100 wamehitimu elimu ya maandalizi msingi na sekondari.