Zenj FM
Zenj FM
6 November 2025, 1:57 pm

Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Raya Issa Mselem, ametangaza matokeo hayo mara baada ya kumalizika kwa zoezi la upigaji kura lililofanyika katika kikao cha kwanza cha Baraza jipya lililofanyika Chukwani, Zanzibar.
Na Mary Julius.
Zuberi Ali Maulid amechaguliwa kwa mara nyingine kuwa Spika wa Baraza la 11 la Wawakilishi Zanzibar kwa kipindi cha mwaka 2025 hadi 2030, baada ya kupata kura 53 kati ya kura 68 zilizopigwa, sawa na asilimia 94.6 ya kura zote.
Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Raya Issa Mselem, ametangaza matokeo hayo mara baada ya kumalizika kwa zoezi la upigaji kura lililofanyika katika kikao cha kwanza cha Baraza jipya lililofanyika Chukwani, Zanzibar.
Kwa mujibu wa Katibu huyo, Afisi ya Baraza la Wawakilishi ilipokea majina manne ya wagombea kutoka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC). Wagombea hao walikuwa Naima Salum Hamad wa UDP, Suleiman Ali Khamis wa ADC, Chausiku Khatibu Mohammed wa NLD, na Zuberi Ali Maulid kutoka CCM.
Mara baada ya kutangazwa mshindi, Spika mteule Zuberi Ali Maulid amewashukuru wajumbe wote wa Baraza pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa imani waliyoonesha kwake.
Ameahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano na kujenga Baraza lenye ufanisi, umoja, na heshima kwa wananchi wote wa Zanzibar.

Baada ya uchaguzi huo, wajumbe wa Baraza la 11 la Wawakilishi waliapishwa kwa kiapo cha uaminifu, chini ya uongozi wa Spika mteule, Zuberi Ali Maulid.