Zenj FM

Jamila Borafya: Mwanamke jasiri anayeinua sauti za wenye Uulemavu

4 November 2025, 9:19 pm

Jamila Borafya Hamza akizungumza katika moja ya warsha alizowahi kuhudhuria.

Si kila anayeshindwa anakata tamaa wengine hufanya kushindwa kuwa ngazi ya mafanikio.”
Jifunze kutoka kwa safari ya Jamila, mwanamke shupavu aliyeamua kuandika ukurasa mpya wa uongozi unaojenga mshikamano na matumaini

Na Ivan Mapunda.

Katika medani ya siasa za Zanzibar, jina la Jamila  Borafya Hamza  limeibuka kama alama ya uthubutu na uongozi jumuishi.

“Mwaka 2020 niligombania  uwakilishi jimbo la Mwanakwereke kupiti viti maalum UWT kupitia watu wenye ulemavu ila jina langu halikurudi  kwenye ngazi ya tawi,na mwaka 2025  niligombania tena  jina langu lilipita kwenye kura za ndani ila lilipoenda kujadiliawa Dodoma halijrudi kwangu mimi ni uthubutu”.

Jamila  ameweka msingi wa uongozi unaoamini katika mshikamano na huduma bora kwa jamii. Safari yake inathibitisha kwamba uongozi siyo hadhi ya mtu binafsi, bali ni wajibu wa kuondoa vikwazo na kufungua njia kwa wengine.

Safari ya maisha na elimu

Jamila Borafya Hamza  amezaliwa mwaka 1997 Kwahani , Wilaya ya mjini , Mkoa wa wa mjini Magharibi Unguja, ni mtoto wa 3 katika watoto wa  tatu na yeye pekee ndio mwenye ulemavu wa macho wa kuzaliwa.

Safari yake ya elimu ilianza mwaka 2004 katika Skuli ya mjumuisho Kisiwandui  Unguja , kisha mwaka 2017 akaendelea na masomo ya sekondari Haile salasi na Mbarali na baadaye  mwaka  2022 alijiunga na chuo cha  Glorious Technology na kuchukua cheti cha biashara ,

Mwaka 2025 alijiunga na  Stashahada ya Usimamizi wa Biashara katika chuo Utawala wa Umma Zanzibar  ambapo anaendelea na masomo , inayoonyesha  dhamira yake ya dhati kuleta mabadiliko ya kweli katika  jamii.

Uzoefu na Uwanachama wa Kisiasa

Jamila ni mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM ) Mwaka 2009 akiwa na miaka kumi na mbili (12) alianzia kwenye mabaraza ya watu wenye ulemavu ,  mwaka 2012 alichaguliwa katika  serikali ya wanafunzi skuli ya Kisiwandui kuwa  waziri wa habari na mwaka 2015 alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Tuseme Club  na mwaka 2016 alishiriki bunge la vijana akiwa kama mjumbe wa kawaida akiwakilisha watu wenye ulemavu na mwaka 2016 alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa baraza la vijana shehia ya mwanakwereke  aliamua kuingia kwenye siasa kupitia CCM ambapo mwaka 2020 aliteuliwa kuwa mjumbe wa kamati ya utekelezaji jmbo la Mwanakwereke, akivutwa na hamasa ya kuwatetea watu wenye ulemavu. Akizungumzia safari yake, Jamila  anasema: “Nilichagua kusimama imara kwa sababu nilijua natetea haki za watu, siyo maslahi binafsi. Nimejifunza kuwa ulemavu si kikwazo, bali ni nguvu ya kuthibitisha kwamba kila mtu ana nafasi ya kuongoza.”
Sababu za Kugombea

Sababu kubwa za kugombani ni ukomavu wa kisiasa kwa sababu nilishapata mafunzo kutoka kwenye taasisi mbali mbali na uwezo  mkubwa ambao  ninao lakini kikubwa ni kutaka kuwatete na kuwa sauti ya watu wenye uleamvu kupiti baraza la wawakilishi ili kuzisemea changamoto zetu.

Changamoto na mafanikio

Safari yake haikuwa rahisi,amekumbana na changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa vifaa vya kazi vinavyohitajika kwa mtu mwenye ulemavu, pamoja na unyanyapaa kutoka kwa baadhi ya watu waliodhani hawezi kumudu nafasi ya uongozi. Lakini hakukata tamaa.

Lakini ndani ya changamoto hiyo,alipata mafanikio makubwa mwanamke huyu ikiwa kupata tunzo mbali mbali za kiongozi bora kijana  pamoja na kuiaminisha jamii kuwa watu wenye ulemavu wanauwezo wa kufanya kitu chochote  na kusimama popote kama walivyowatu wa kawaida
Ushauri Kwa Wanawake

Kwa ujasiri wake, Jamila  anaendelea kusimama kama sauti ya matumaini kwa wanawake na watu wenye ulemavu. Amekuwa akisisitiza: “Kila mtu ana nafasi yake kwenye siasa na maendeleo ya nchi, tusikubali kunyanyapaliwa au kuonekana hatuna uwezo. Tukisimama pamoja, tunaweza kufanikisha mambo makubwa.”

Safari ya Jamila Borafya Hamza  inabaki kuwa ushuhuda kwamba mwanamke mwenye ulemavu anaweza kusimama na kuwa kiongozi thabiti – kiongozi wa jamii, familia na taifa.