Zenj FM

Maisha Meds, Wizara ya Afya waungana huduma za macho Zanzibar

7 October 2025, 5:16 pm

Wananchi visiwani Zanzibar wakipatiwa huduma za kupima macho na kukabidhiwa miwani bure katika viwanja vya Mnazi mmoja Zanzibar zoezi lililo endeshwa na Wizara ya Afya na Taasisi ya Maisha Meds.

Na Mary Julius.

Katika kuadhimisha Siku ya Uoni Hafifu Duniani, Wizara ya Afya Zanzibar kwa kushirikiana na Maisha MedsnaPondeza Foundation wameandaa zoezi maalumu la upimaji wa macho litakalofanyika katika Jimbo la Chumbuni na Jimbo la Mtoni.

Zoezi hilo la siku mbili kwanzia tarehe 8 hadi tarehe 9  linalenga kutoa huduma ya bure ya uchunguzi wa macho na ugawaji wa miwani kwa wananchi wenye umri kuanzia miaka 40 na kuendelea.

Akizungumza na Zenj FM, Mratibu wa Huduma ya Macho Kitaifa,kutoka wizara ya afya Zanzibar  Dkt Fatma Said Ali, amesema kambi hizo zimeandaliwa ili kuhamasisha wananchi kupima macho mara kwa mara, hasa wale waliofikia umri wa miaka 40 na zaidi, ambapo changamoto za kuona huanza kujitokeza kama ilivyo kwa maradhi mengine ya kudumu kama vile kisukari na shinikizo la damu.

Aidha dkt fatuma amewaomba Wananchi kufika katika Mabanda ya Ng’ombe  kwa jimbo la Chumbuni na viwanja vya mpira vya Kibweni kwa jimbo la Mtoni kwa ajili ya kupata huduma hizo bure.

Sauti ya Mratibu wa Huduma ya Macho Kitaifa,kutoka wizara ya afya Zanzibar  Dkt Fatma Said Ali.

Kwa upande wake, Juma Bashiri Juma, mfanyakazi wa Maisha Meds, amesema taasisi hiyo inashirikiana na Wizara ya Afya kuhakikisha jamii ya Zanzibar inapata huduma bora za macho ikiwemo upimaji bure, utoaji wa miwani na dawa kwa wagonjwa watakaobainika kuwa na matatizo ya macho.

Sauti ya Juma Bashiri Juma, mfanyakazi wa Maisha Meds.

Aidha amesema Lengo la taasisi hiyo  ni kuwafikia angalau watu 1,000 kupitia kampeni hiyo.

Sauti ya Juma Bashiri Juma, mfanyakazi wa Maisha Meds.

Siku ya Uoni Hafifu Duniani huadhimishwa kila Alhamisi ya pili ya mwezi Oktoba, ikiwa na dhamira ya kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa uoni bora na upimaji wa macho mara kwa mara.