Zenj FM
Zenj FM
6 October 2025, 5:33 pm

Na Mary Julius.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani kutoka Jumuiya ya Maradhi ya Moyo Zanzibar, Dkt. Ahlam Ali Amour, ameitaka jamii kujenga utaratibu wa kupima afya mara kwa mara ili kujiepusha na maradhi ya moyo pamoja na yale yasiyoambukiza.
Akizungumza katika zoezi la upimaji wa afya kwa watu wenye ulemavu lililodhaminiwa na Jumuiya ya Maradhi ya Moyo Zanzibar kwa kushirikiana na Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar (UWZ), ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani, Dkt. Ahlam amesema wamelenga kuwasogezeqa huduma hizi watu wenye ulemavu kwa sababu licha ya changamoto zao za kimwili, wengi wao pia wako hatarini kupata maradhi yasiyoambukiza, ikiwemo shinikizo la damu na matatizo ya moyo.
Amefafanua kuwa takwimu zinaonyesha kila watu watatu, mmoja ana tatizo la shinikizo la damu, hivyo ni muhimu kwa jamii kuzingatia lishe bora, kufanya mazoezi, na kupima afya mara kwa mara ili kujikinga na maradhi hayo.
Aidha Dkt. Ahlam amezitaka taasisi mbalimbali kuendelea kuwaangalia kwa jicho la huruma watu wenye ulemavu kwa kuwasogezea huduma za afya karibu na jamii wanazoishi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar Abdulwakili H Hafidhi ameishukuru Jumuiya ya Maradhi ya Moyo kwa kuanzisha mpango huo, akisema kuwa watu wengi wenye ulemavu hawana utamaduni wa kupima afya zao kutokana na changamoto za upatikanaji wa huduma.
Naye Meneja wa Jumuiya ya Wanaoishi na Maradhi Yasiyoambukiza, Haji Khamis, amezitaka taasisi nyingine kuungana katika juhudi hizi ili watu wengi zaidi wapate fursa ya kupima afya zao na kuishi kwa kuzingatia hali zao za kiafya.
Nao Walionufaika na huduma hizo wameishukuru jumuiya kwa kuwapima na kuwapa ushauri wa kiafya, wamesema hatua hiyo imewasaidia kuelewa afya zao na kuchukua tahadhari mapema.
Kila ifikapo tarehe 29 Septemba, dunia huadhimisha Siku ya Moyo Duniani ambapo kwa mwaka huu, Jumuiya ya Maradhi ya Moyo Zanzibar imeadhimisha siku hiyo kwa kuwapatia huduma za afya watu wenye ulemavu.