Zenj FM
Zenj FM
25 August 2025, 4:17 pm

Na Zulfa Shaibu Mkanjaluka.
Mrundikano wa taka katika Shehia ya Chunga, Zanzibar, umeibuka kuwa changamoto kubwa kwa wakazi wa eneo hilo, wakihusisha hali hiyo na ongezeko la maradhi ya milipuko kama kipindupindu na mazingira machafu kwa ujumla.
Katika mahojiano na Zenji FM Radio, baadhi ya wananchi wa Shehia ya Chunga wameeleza kuwa hali ya taka kutokusafirishwa kwa wakati si tu kwamba inahatarisha afya zao, bali pia inaleta usumbufu mkubwa wa maisha ya kila siku.
Aidha wameeleza kuwa ushindani wa ulipaji wa fedha za magari ya taka ni changamoto nyingine inayokwamisha juhudi za kuondoa taka hizo kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Sheha wa Shehia ya Chunga, Karume Ali, amesema kuwa tangu mwaka 2017, wameanzisha utaratibu wa kuondoa taka kwa kushirikiana na vijana wa usafi.
Aidha Sheha amesema kwa sasa, vijana 26 wamewekwa rasmi kusaidia katika zoezi la kubeba taka kutoka vituo mbalimbali na kuzifikisha katika maeneo rasmi ya kutupia taka.