Zenj FM
Zenj FM
20 August 2025, 7:37 pm

Na Mary Julius.
Afisa Uhusiano wa Mpango wa Damu Salama, Ussi Bakar Mohamed, amesema Serikali ya awamu ya Nane imefanya maboresho katika sekta ya afya kwa kujenga hospitali katika kila wilaya, hatua inayoongeza mahitaji ya damu salama kwa wagonjwa mbalimbali.
Ameyasema hayo katika bonanza la kuchangia damu lililofanyika katika viwanja vya Mapinduzi Square Kisonge amesema jamii inapaswa kuwa na moyo wa kujitolea kuchangia damu kwa hiari ili kuhakikisha hospitali hizo zinaendelea kutoa huduma bora, hasa kwa wagonjwa wa dharura, akinamama wajawazito, na watoto wachanga.
Aidha, Ussi amevitaka vyombo vya habari kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wakisisitiza kuwa bado kuna uhitaji mkubwa wa elimu ya kutosha kuhusu suala hilo.
Nae, Meneja wa Damu Salama kutoka Zenj Holding Ltd, Dkt. Riziki Omar Ali , amesema moja ya malengo makuu ya taasisi hiyo ni kuratibu mabonanza ya uchangiaji damu ili kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa damu hospitalini.
Amesema mabonanza hayo ni sehemu ya mikakati endelevu wa kusaidia sekta ya afya, ambapo jamii itahamasishwa kushiriki moja kwa moja katika shughuli za uchangiaji damu kwa hiari.
Kwa upande wake Meneja Mahusiano wa Shirika la Bandari Hassan Juma Amour amesema Shirika la Bandari wameungana na Zenj Holding Ltd kuandaa kampeni ya kuwashajihisha vijana ili waweze kuchangia damu.
Wakizungumza mara baada ya kuchangia damu katika Viwanja vya Kisonge ,baadhi ya wananchi amesema jamii inapaswa kutambua kuwa damu ni hitaji la kila siku, na kuchangia damu ni njia mojawapo ya kuokoa maisha ya waatu wanaohitaji huduma hiyo muhimu.