Zenj FM

Zanzibar yapiga hatua muhimu kuelekea uchumi wa kidijitali kufikia 2030

15 August 2025, 8:09 pm

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Dk. Khalid Salum Mohamed akiwa na Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Airtel Tanzania Charles Mustafa Kamoto katika hafla ya utiaji saini kati ya ZICTIA na Airtel.

Na Mary Julius.

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Dk. Khalid Salum Mohamed amesema hatua ya kutiwa saini makubaliano ya ushirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia ZICTIA, Zanzibar Communication Corporation na kampuni ya Airtel ni hatua muhimu katika kuhakikisha huduma bora za mawasiliano zinapatikana visiwani Zanzibar.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini huo,uliofanyika katika ukumbi wa wizara hiyo Kisauni Zanzibar Waziri amesema Serikali imeweka kipaumbele katika kukuza na kuimarisha sekta ya mawasiliano, kwani dunia kwa sasa inakwenda kwa kasi katika teknolojia na Zanzibar haiwezi kubaki nyuma.
Waziri Dkt. Khalid amesema Serikali imewekeza katika miundombinu ya mawasiliano kwa kujenga zaidi ya minara 45, lengo likiwa ni kusogeza huduma bora kwa wananchi .
Waziri amesema kuimarika kwa mawasiliano kutasaidia katika kuvutia wawekezaji na kukuza utalii, kwani watalii wengi hupendelea kuwa na mawasiliano bora wanapowasili nchini.
Aidha, amesema mageuzi haya yatachangia pia kuboresha elimu, kuimarisha huduma za kijamii, na kuinua uchumi wa kidijitali ifikapo mwaka 2030.

Sauti ya Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Dk. Khalid Salum Mohamed.

Nae , Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Zanzibar, Shukuru Awadh Suleiman, amesema ushirikiano wa muda mrefu wa ZICTIA na kampuni ya Airtel umezaa matunda, ikiwa ni pamoja na kuongeza upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika skuli za Unguja na Pemba, ambapo kwa awamu ya kwanza skuli 100 zitapatiwa huduma hiyo bure.

Sauti ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Zanzibar, Shukuru Awadh Suleiman.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Airtel Tanzania Charles Mustafa Kamoto ameshukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano huo na kuahidi kuongeza juhudi katika kuboresha huduma za mtandao visiwani humo.
Amesema makubaliano haya yataongeza upatikanaji wa huduma, kuimarisha usalama mtandaoni, na kusaidia katika utoaji wa elimu ya kidijital.

Sauti ya Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Airtel Tanzania Charles Mustafa Kamoto.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Dkt Habiba Hassan Omar amesema makubaliano haya ni matokeo ya mawasiliano ya muda mrefu kati ya ZICTIA na Airtel, na kwamba ni msingi wa kuifikisha Zanzibar katika uchumi wa kidigital.

Sauti ya Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Dkt Habiba Hassan Omar.