Zenj FM
Zenj FM
24 July 2025, 1:12 pm

Na Mary Julius.
Afisa Elimu kwa Umma kutoka Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA), Sada Salum Issa, amezitaka taasisi za umma na binafsi kushirikiana na mamlaka hiyo kwa kutoa taarifa pale wanapobaini viashiria vya rushwa au uhujumu uchumi katika maeneo yao ya kazi,lengo ni kusaidia kuyatokomeza matendo hayo ambayo yanadhoofisha maendeleo ya jamii.
Sada ametoa wito huo wakati wa mafunzo maalum yaliyotolewa na ZAECA kwa viongozi wa Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar UWZ , ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya ZAECA ya kutoa elimu juu ya athari na madhara ya rushwa katika taasisi mbalimbali visiwani Zanzibar.
Amesema ushirikiano kutoka kwa taasisi binafsi na za serikali ni muhimu ili hatua stahiki zichukuliwe mapema, na kuhakikisha matendo hayo hayaendelei kushamiri nchini.
Aidha, amesema kuelekea Uchaguzi Mkuu, ZAECA imejiandaa kwa mikakati mbalimbali ya kupambana na rushwa na uhujumu uchumi, kwa kutoa elimu kwa jamii ili wajiepushe kujiingiza katika vitendo hivyo hasa katika kipindi hiki nyeti.
Kwa upande wao, wafanyakazi wa Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar UWZ wameeleza kufarijika kwao kupatiwa mafunzo hayo, wakisema yatasaidia katika kuzuia vitendo vya rushwa ndani ya jumuiya yao.
Aidha Wameiomba ZAECA kuendeleza kutoa elimu kwa makundi mengine, hasa vijana watu wenye ulemavu na watu wasio na ajira, ambao mara nyingi huwa waathirika wakubwa wa vitendo vya rushwa.