Zenj FM

TRA yachangia ukuaji wa uchumi Zanzibar makusanyo yafikia bil. 647.25

19 July 2025, 5:19 pm

Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya Salum, akizungumza wakati akifungua kikao kazi cha tathmini ya utendaji wa TRA kwa mwaka wa fedha 2024/2025, kilichofanyika katika Ukumbi wa Madinat Al Bahr, Zanzibar.

Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya amesema bila ya uwepo wa TRA, serikali zote mbili — ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi ya Zanzibar — zisingeweza kutekeleza mipango ya maendeleo.

Na Mary Julius.

Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya Salum, amesema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ni taasisi muhimu inayochochea maendeleo ya kiuchumi ya Tanzania Bara na Zanzibar, kutokana na mchango wake mkubwa katika ukusanyaji wa mapato ya taifa.

Dkt. Saada ameyasema hayo wakati akifungua kikao kazi cha tathmini ya utendaji wa TRA kwa mwaka wa fedha 2024/2025, kilichofanyika katika Ukumbi wa Madinat Al Bahr, Zanzibar.

Sauti ya Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya.

Aidha, Waziri ameipongeza TRA kwa kuvuka lengo la makusanyo ya mapato kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kwa asilimia 27, akibainisha kuwa mafanikio hayo hayawezi kufikiwa bila weledi wa watumishi wa TRA na uelewa mkubwa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kulipa kodi.

Amesema elimu kwa walipakodi imechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza hiari ya ulipaji kodi, hali iliyowezesha kuongeza mapato ya ndani.

Sauti ya Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya.

Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa TRA,Yusuph Juma Mwenda amesema kikao kazi hicho ni jukwaa muhimu kwa TRA kutathmini mafanikio na changamoto zilizojitokeza mwaka uliopita, pamoja na kupanga mikakati ya ufanisi kwa mwaka wa fedha 2025/2026. Kamishna amesisitiza huduma bora kwa wateja (customer care) na mahusiano ya karibu na walipakodi ni msingi wa ufanisi katika ukusanyaji wa mapato, huku akiwapongeza wafanyabiashara na wananchi wa Zanzibar kwa kulipa kodi kwa hiari.

Sauti ya Kamishna Mkuu wa TRA,Yusuph Juma Mwenda.

Naye Naibu Kamishna Mkuu wa TRA – Zanzibar Saleh Haji Pandu ameipongeza timu ya TRA Zanzibar kwa kufanikisha ukusanyaji wa mapato kwa kiwango cha asilimia 107.86, ambapo jumla ya shilingi bilioni 647.25 zilikusanywa mwaka uliopita.
Amesema ushirikiano kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar umechangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha matokeo hayo, na kueleza matumaini ya kuendeleza mafanikio hayo katika mwaka wa fedha 2025/2026.
Aidha ametoa wito kwa washiriki wa kikao hicho kuchangia kwa dhati mawazo na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha zaidi mifumo na mikakati ya ukusanyaji wa mapato nchini.

Sauti ya Naibu Kamishna Mkuu wa TRA – Zanzibar Saleh Haji Pandu.