Zenj FM

Kadi za matibabu za kidijitali zaipa Zanzibar tuzo ya kimataifa

13 July 2025, 7:05 pm

Waziri wa Afya wa Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui akiwa ameshikilia Tuzo ya kimataifa ya World Summit on the Information Society (WSIS)U uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume

Tuzo ya World Summit on the Information Society (WSIS) hutolewa na International Telecommunication Union (ITU) kwa kutambua matumizi bora ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika maendeleo ya jamii. Mradi wa Kadi ya Matibabu ya Zanzibar uliibuka miongoni mwa miradi bunifu iliyopewa heshima hiyo mwaka huu.

Na Mary Julius.

Waziri wa Afya wa Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, amesema tuzo ya kimataifa ya World Summit on the Information Society (WSIS) ni uthibitisho wa dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kujenga mfumo wa afya jumuishi unaotegemea teknolojia ya kisasa kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wote kwa usawa.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume mara baada ya kurejea na tuzo hiyo iliyotolewa mjini Geneva, Uswizi, Waziri Mazrui amesema mafanikio hayo ni matokeo ya uongozi madhubuti, ushirikiano wa kimkakati na taasisi ya PharmAccess, pamoja na juhudi kubwa za watumishi wa afya nchini.
Amesema tuzo hiyo ni ushahidi wa kutambuliwa kwa juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha huduma za afya kwa kutumia teknolojia, kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa matibabu kwa wananchi wote bila ubaguzi.

Sauti ya Waziri wa Afya wa Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui,

Aidha, Waziri Mazrui ameipongeza PharmAccess kwa kushirikiana kwa karibu na Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (CHWs), ambao walisimamia zoezi la usajili wa wananchi nyumba kwa nyumba, na kusisitiza umuhimu wa kujifunza teknolojia na kutumia akili mnemba ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya dunia.

Aidha Mazrui amesema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na PharmAccess imefanikiwa kuwasajili asilimia 93 ya wananchi wa Zanzibar na kuwapatia kadi za matibabu, zinazowawezesha kupata matibabu bure katika hospitali na vituo vya afya vilivyo karibu nao.

Sauti ya Waziri wa Afya wa Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui’
Waziri wa Afya wa Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui akiwa ameshikilia Tuzo ya kimataifa ya World Summit on the Information Society (WSIS)U uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Programu wa PharmAccess,Zanzibar Faiza Bwanakheri Abbas, amesema tuzo hiyo inalenga kutambua juhudi za serikali na mashirika mbalimbali katika kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, hasa kupitia matumizi ya mifumo ya kisasa ya bima na kadi za matibabu.

Sauti ya Mkurugenzi wa Programu wa PharmAccess,Zanzibar Faiza Bwanakheri.