Zenj FM
Zenj FM
10 July 2025, 6:17 pm

Mradi wa Zanzadapt, unalenga kuimarisha nafasi ya mwanamke kiongozi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na unatekelezwa kwa ushirikiano wa TAMWA ZNZ, Jumuiya ya Misitu Pemba (CFP), Jumuiya ya Misitu Kimataifa (CFI), kwa kushirikiana na Ubalozi wa Canada.
Na Mwandishi wetu.
Meneja Miradi kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ), Nairat Abdulla amewaomba wanawake kutumia vyombo vya habari, hasa mitandao ya kijamii, kwa lengo la kutangaza kazi wanazozifanya katika nyanja mbalimbali, ikiwemo mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili kwa wakulima viongozi kutoka shehia nne za Mkoa wa Kusini Unguja (Bungi, Unguja Ukuu, Uzi na Ng’ambwa), yaliyofanyika katika ofisi za TAMWA-ZNZ Tunguu, Nairat amesema wanawake wanafanya kazi kubwa kwenye uzalishaji na utunzaji wa mazingira lakini sauti zao bado hazisikiki vya kutosha.
Naye Meneja Mawasiliano wa TAMWA-ZNZ, Sofia Ngalapi amesisitiza kuwa wanawake wakulima wana mchango mkubwa katika kuhifadhi mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, hivyo ni vyema wakatangaza kazi zao ili kuhamasisha jamii nzima.
Afisa Mawasiliano wa TAMWA-ZNZ, Khairat Haji, amewataka washiriki kutumia mitandao ya kijamii kwa uangalifu kama nyenzo ya kujitangaza na kujiongezea kipato, huku wakiepuka kuchapisha taarifa za maisha binafsi kwa usalama wao.
Nao Wakulima hao wamelezea kufarijika na mafunzo hayo kupitia programu ya Zanzadapt, wakiahidi kuwa mabalozi katika jamii zao.
Mradi huu unahusisha maeneo ya uhifadhi wa mikoko, kilimo mseto, uongozi wa wanawake na masuala ya jinsia.