Zenj FM
Zenj FM
9 July 2025, 5:49 pm

Mary Julius.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar ambaye pia ni Makamo Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Jaji Aziza Iddi Suwed ametoa wito kwa wajumbe wa kamati hiyo kushiriki kikamilifu kwa kutoa maoni yao ili kusaidia kutungwa kwa kanuni madhubuti za maadili zitakazotumika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Akizungumza katika kikao cha uzinduzi rasmi wa Kamati ya Maadili Kitaifa iliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Tume ya Uchaguzi , Wilaya ya Magharibi A, Mwera Mwenyekiti Aziza amesema maoni yatakayotolewa na wajumbe katika kikao hicho ni msingi muhimu wa kutengeneza nyaraka bora ya maadili itakayozingatia misingi ya haki, usawa na amani wakati wa uchaguzi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Thabit Idarous Faina amesema kikao hicho ni sehemu ya mchakato wa kushirikisha wadau wa uchaguzi ili kuandaa kanuni ya maadili, kama inavyoelekezwa na sheria ya Tume, Amesema maadili hayo yatapitishwa na vyama vya siasa kabla ya kuanza rasmi kwa kampeni za uchaguzi.
Aidha, amesema chama chochote kitakachokataa kusaini kanuni hizo hakitaruhusiwa kufanya kampeni, ingawa bado kitakuwa na haki ya kushiriki uchaguzi mkuu.
Kwa upande wake Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Khamis Mbeto , amesema uwepo wa kanuni hizo zitasaidia katika kuongoza zoezi zima la Uchaguzi na kuwaomba wadau wa kisiasa kuzikubali na kuzisimamia kwa pamoja kama watakavyo kubaliana na kusaini.
Nao Makamu Mwenyekiti wa chama cha ADA-TADEA, Ali Makame Issa, na Katibu Mkuu wa chama cha MAKINI, Amir Hassan Amir, kwa pamoja wamesema mkutano huo unaonyesha dhamira njema ya kuhakikisha kila chama kinasimamia maadili, ili uchaguzi uwe wa amani na mshikamano kwa maslahi ya taifa.