Zenj FM

Zanzibar yawasha moto tena Afrika tuzo ya pili mfululizo WTA

1 July 2025, 3:27 pm

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrik Ramadhan Soraga, akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa wizara hiyo uliopo Kikwajuni, Zanzibar.

Tuzo za World Travel Awards,hushirikisha makundi mbalimbali katika sekta ya utalii, ikiwa ni pamoja na hoteli, viwanja vya ndege, mashirika ya ndege, vivutio vya kitalii, waandaaji wa matukio na tamasha, na huduma nyingine zinazohusiana na usafiri na ukarimu.

Na Mary Julius.

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrik Ramadhan Soraga, amesema Zanzibar imeendelea kung’ara kimataifa kwa kushinda tena tuzo ,katika hafla ya World Travel Awards (WTA) iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Wizara hiyo uliopo Kikwajuni, Zanzibar, Waziri Soraga amesema ushindi huo ni matokeo ya juhudi kubwa za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Kamisheni ya Utalii Zanzibar kwa kushirikiana kwa karibu na wadau mbalimbali wa sekta ya utalii.
waziri amesema Tuzo za World Travel Awards, ambazo zilianzishwa mwaka 1993, zinatambuliwa duniani kote kama kipimo cha ubora katika sekta ya usafiri, utalii na ukarimu.
Zanzibar imepata ushindi huu kwa mara ya pili mfululizo – mwaka jana na mwaka huu – ikiipiku nchi kubwa barani Afrika kama Ghana, Afrika Kusini, Rwanda (Kigali), na Kenya.

Sauti ya Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrik Ramadhan Soraga.

Aidha, Waziri Soraga ametumia fursa hiyo kuarifu kuwa hafla ya kilele ya Global Ceremony ya World Travel Awards kwa mwaka 2026 inatarajiwa kufanyika hapa Tanzania, na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inafanya juhudi kuhakikisha hafla hiyo ya heshima ya kimataifa ifanyike visiwani Zanzibar.

Sauti ya Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrik Ramadhan Soraga.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wawekezaji wa Utalii Zanzibar (ZATI), Suleiman Ali Mohammed, amesema mafanikio haliyo patikana yanaakisi maono ya uongozi wa juu wa nchi, hususan Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Aidha, amewashukuru wananchi wa Zanzibar kwa mchango wao katika kukuza utalii na kutoa wito kwa wawekezaji kuhakikisha wanawajali na kushirikisha wananchi wa maeneo wanayowekeza ili nao waweze kunufaika moja kwa moja na uwekezaji huo.

Sauti ya Mwenyekiti wa Chama cha Wawekezaji wa Utalii Zanzibar (ZATI), Suleiman Ali Mohammed,