Zenj FM
Zenj FM
22 June 2025, 5:06 pm

Na Mary Julius.
Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wajane Zanzibar, Tabia Makame Mohammed, amesema kuwa moja ya changamoto kubwa zinazowakumba wajane ni msongo wa mawazo, unaosababishwa na kukosekana kwa malezi na matunzo kwa watoto.
Akizungumza na Zenj FM, Tabia amesema hali hiyo inatokana na baadhi ya wanaume wanapoachana na wake zao kukwepa majukumu ya ulezi, na hivyo kuwaacha wanawake kubeba mzigo wa kulea watoto peke yao.
Amesema licha ya juhudi za kuwawezesha wanawake kiuchumi, bado suala la malezi linahitaji kupewa kipaumbele cha pamoja kati ya wazazi wote wawili.
Aidha, Tabia ameiomba Wizara ya Maendeleo ya Jamii na Jinsia kuhakikisha kuwa wanaume wanawajibika ipasavyo katika malezi ya watoto, huku akisisitiza kuwepo kwa maelewano kati ya mama na baba kwa ajili ya ustawi wa mtoto.
Kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu,Mkurugenzi Tabia amewasihi wakina mama wajane kushiriki kikamilifu katika siasa, kwa kujiunga na vyama na kuwania nafasi za maamuzi ili kutilia mkazo sheria zitakazotetea haki za watoto na wajane.
Kila ifikapo june 23 dunia huadhimisha Siku ya Wajane Duniani , kwa upande wa Tanzania Bara Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum anatarajiwa kuadhimisha siku hiyo katika mikoa yote, huku maadhimisho rasmi ya kitaifa yatafanyika mkoani Iringa, sambamba na uzinduzi wa Mwongozo wa Uratibu wa Wajane Tanzania 2025.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Tuimarishe Fursa za Kiuchumi Kuchochea Maendeleo ya Wajane.”