Zenj FM

Wandishi wa habari ripotini ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake

18 June 2025, 7:50 pm

Mkurugenzi wa Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA ZNZ ) Dk Mzuri Issa akizungumza katika mafunzo ya siku moja, yaliyofanyika katika ofisi ya chama hicho huko Tunguu.

Na Ivan Mapunda

Wandishi wa habari nchini wametakiwa kutumia kalamu zao vizuri kuandika kurepoti na kukemea taarifa za ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake watakaogombea nafasi mbali mbali za uongozi katika kipindi hiki cha uchaguzi.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA ZNZ ) Dk Mzuri Issa katika mafunzo ya siku moja, yaliyofanyika katika ofisi ya chama hicho huko Tunguu,na kuwashirikisha wandishi wa vyombo mbali mbali vya habari.
Dk Mzuri, amesema kuelekea kipindi cha uchaguzi wandishi wa habari wana jukumu kubwa la kufanya kazi yao ya ulinzi ili kuwalinda wagombea wanawake watakaogombea nafasi mbali mbali za uongozi dhidi ya vurugu na udhalilishaji unaotokea katika kipindi hicho.

Sauti ya Mkurugenzi wa Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA ZNZ ) Dk Mzuri Issa.

Nae, Afisa Khairat Haji Kutoka TAMWA Znz, amesema ni vyema wandishi wa habari kuelewa pia udhalilishaji unaofanyika katika mitandao ya kijamii na kuweza kukemea .
Amesema, imezoeleka katika mitandao mbali mbali ya kijamii mwanamke akiweka kitu mfano, picha yake basi watu hawaangalii kile alichokiweka wataanza kumzodoa yeye na muonekano wake na huo pia ni udhalilishaji wa kimtandao.
Mafunzo hayo , maalum ya siku moja yameandaliwa na Chama Cha Wandishi Wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar ( TAMWA ZNZ) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu Cha Dar Es Salaam ( UDSM) yamewashirikisha wandishi wa habari 30 wa Zanzibar kwa lengo la kuripoti na kukemea ukatili wa wanawake kipindi cha uchaguzi.