Zenj FM

Ajali ya moto yaua kijana Michamvi, mke ashikiliwa kwa uchunguzi

8 June 2025, 4:39 pm

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP. Daniel Shillah .

Na Mary Julius.

Khamis Rashid Khamis, mwanaume mwenye umri wa miaka 26 na mkazi wa Michamvi Pingwe, Wilaya ya Kusini Unguja, amefariki dunia baada ya kuungua kwa moto akiwa amelala ndani ya nyumba yake ya makuti, tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia tarehe 8 Juni.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP. Daniel Shillah amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha moto huo ni mshumaa uliokuwa ukitumika kama chanzo cha mwanga ndani ya nyumba hiyo.
Kamanda Shillah amesema Jeshi la Polisi linachunguza kwa kina mazingira ya tukio hilo, hasa ikizingatiwa kuwa usiku wa tukio, marehemu anadaiwa kuwa na ugomvi wa kifamilia na mke wake,hivyo mke wa marehemu anashikiliwa na Polisi kwa mahojiano zaidi, ili kubaini iwapo kuna dalili yoyote ya kushiriki katika tukio hilo.

Sauti ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP. Daniel Shillah.

Kamanda Daniel , ametoa wito kwa wananchi kuwa waangalifu na matumizi ya vyanzo vya moto kama mishumaa, hasa katika nyumba za nyasi au makuti, ambazo ni rahisi kushika moto na kusababisha madhara makubwa ya kiutu na mali.

Sauti ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP. Daniel Shillah.