Zenj FM

BIG-Z yawezesha mafunzo ya kuboresha ukusanyaji mapato Zanzibar

26 May 2025, 4:35 pm

Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Zainab Khamis Kibwana akifungua mafunzo ya siku nne ya kujenga uwezo wa fedha za mamlaka za serikali za mitaa kupitia Mradi wa Ukuzaji wa Uchumi Jumuishi Zanzibar BIG-Z.

Na Mary Julius.

Washiriki mafunzo ya kujenga uwezo wa fedha za mamlaka za serikali za mitaa wametakiwa kuyatumia vema mafunzo hayo ili kujiongezea ujuzi ambao utasaidia kuboresha utendaji kazi na kuongeza ufanisi katika maeneo yao ya kazi.
Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Tawala za Mikoa  Zainab Khamis Kibwana ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku nne ya kujenga uwezo wa fedha za mamlaka za serikali za mitaa kupitia mradi wa ukuzaji wa uchumi jumuishi Zanzibar BIG-Z yaliyo fanyika katika hotel ya Golden Tulip uwanja wa ndege Zanzibar.
Amesema Mafunzo haya yamelenga kuimarisha uwezo wa ukusanyaji mapato katika halmashauri za Unguja na Pemba, kuboresha uandaaji wa makisio sahihi na usimamizi bora wa fedha, kuongeza matumizi ya takwimu za kifedha na kijiografia katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Aidha Mkurugenzi Zainab ameishukuru Ofisi ya Rais – Fedha na Mipango, kwa kushirikiana na washiriki wa maendeleo, Benki ya Dunia (World Bank), kwa kuandaa mafunzo hayo.

Sauti ya Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Zainab Khamis.

Mratibu wa Miundo ya Taasisi za Fedha na Teknolojia kutoka BIG-Z, Mohammed Zahran amesema mradi huo umelenga kuimarisha ufanisi katika ukusanyaji wa mapato kwa kutumia teknolojia bora na kuwajengea uwezo watendaji wa serikali za mitaa.
Aidha, amesema mradi unalenga kuangalia namna bora ya kusaidia serikali za mitaa ili kubuni vyanzo vipya vya mapato vya kudumu.

Sauti ya Mratibu wa Miundo ya Taasisi za Fedha na Teknolojia kutoka BIG-Z, Mohammed Zahran.

Kwa upande wake Mkufunzi wa mafunzo hayo, Siasa Mzenzi, amesema halmashauri nyingi nchini zimekuwa zikikumbwa na matatizo ya vyanzo hafifu vya mapato pamoja na changamoto za kiutawala.

Aidha Mzenzi ametoa wito kwa viongozi wa halmashauri kushirikiana kwa karibu na wataalamu wa mipango miji ili kuhakikisha vyanzo vipya vya mapato vinatambuliwa na kuendelezwa.

Sauti ya Mkufunzi wa mafunzo hayo, Siasa Mzenzi.

Nao Washiriki wa mafunzo hayo wameahidi kuyatekeleza mafunzo wanayopata kwa lengo la kuboresha ukusanyaji wa mapato katika halmashauri zao.

Sauti ya washiriki.