Zenj FM

Naibu Waziri Chillo atoa wito kwa wasanii kuenzi maadili ya kitanzania

5 May 2025, 2:16 pm

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Khamis Hamza Chillo akiwa na viongozi wa DCMA na viongozi mbalimbali wa serikali katika uzinduzi wa albamu ya AMKA uzinduzi ulio fanyika katika ukumbi wa Idrisa Abdulwakil.

Na Mary Julius.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Khamis Hamza Chillo, amewataka wasanii nchini kuhakikisha kazi zao za sanaa zinazingatia hulka, silka, na utamaduni wa Kitanzania, hususan wa Kizanzibari, pamoja na kuhimiza amani na mshikamano wa kitaifa.

Akizungumza katika uzinduzi wa albamu mpya ya msanii Tryphon Evarist iitwayo Amka, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Idrisa Abdulwakil, Kikwajuni Zanzibar, Chillo amesema serikali inathamini sanaa, lakini inasisitiza umuhimu wa maudhui yanayojenga jamii badala ya kuyavuruga maadili.

Naibu waziri amempongeza msanii Evarest kwa kazi zake zinazozingatia maadili ya Kizanzibari, amesema ni mfano mzuri kwa wasanii chipukizi.

Aidha Naibu waziri Chillo amekipongeza Kituo cha Muziki cha cha DCMA kwa mchango wanao utoa katika kukuza vipaji vya watoto, hasa wa kike, na kuwasaidia kujiendeleza katika fani ya muziki kwa njia inayowiana na maadili ya jamii.

Sauti ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Khamis Hamza Chillo

Akizungumza katika uzinduzi wa albamu Amka, Mkurugenzi wa Kituo cha Muziki cha DCMA (Dhow Countries Music Academy), Halda Mohamed Alkanaa, amempongeza msanii Tryphon kwa kuonesha nidhamu, ubunifu, na uhalisia katika kazi yake ya sanaa Alkanaa amesema uzinduzi wa albamu hiyo uwe ni mwanzo wa mafanikio makubwa kwa Tryphone .

Aidha amesema dhamira ya chuo cha DCMA ni kuendelea kulea vipaji kwa misingi ya maadili, utamaduni, na ubora wa muziki wa Kiafrika, hususan ule wa Kizanzibari.

Hafla hiyo imehudhuriwa na wadau mbalimbali wa muziki, viongozi wa serikali, pamoja na mashabiki wa Tryphon, ambapo aliwasilisha nyimbo zote kumi zilizopo katika albamu yake mpya.