Zenj FM
Zenj FM
22 April 2025, 7:24 pm

Na Mary Julius.
Kituo cha Muziki cha DCMA (Dhow Countries Music Academy) kimesema kinashirikiana na msanii Trypon Evarist katika kuandika muziki wa zamani wa Zanzibar kwa lengo la kuuhifadhi na kuutunza, ili vizazi vijavyo viweze kuutumia katika hali yake halisi.
Ushirikiano huu wa msanii Trypon Evarist na mwalimu Thabit Omary unatarajiwa kuleta mchango mkubwa katika kuhifadhi historia ya muziki wa kale, huku wakitumia mbinu za kitaalamu kuhakikisha kuwa muziki huu hausahauki wala kupotea.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa chuo hicho ikiwa ni kuelekea uzinduzi wa albamu yake ya kwanza “Amka”, may 3 Trypon Evarist amesema moja ya changamoto kubwa ni wasanii wa Zanzibar kutoona thamani ya muziki wa asili yao, wakihisi kuwa hauna soko la kimataifa.
Trypon mwenye uzoefu wa miaka kumi na miwili katika kujifunza muziki, amesema amekumbana na changamoto nyingi zikiwemo kudharauliwa na watu kwa sababu ya mwelekeo wake wa kuimba muziki wa asili.
Aidha Trypon Evarist ametoa wito kwa wasanii wa Zanzibar kuthamini urithi wao wa kitamaduni kwa kuendeleza muziki wa asili ya Kizanzibari.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa DCMA Halda Mohamed Alkanaa amesema chuo hicho kimemsaidia msanii huyo hadi kukamilika kwa albamu yake, ambayo ina jumla ya nyimbo kumi.
Nae mjumbe wa bodi ya chuo hicho Mohamed Muombwa amewataka Wazanzibari kutambua na kuthamini utajiri wa muziki wao wa asili, kwani ni sehemu muhimu ya utambulisho wao wa kitamaduni.
Albamu hiyo inatarajiwa kuzinduliwa rasmi siku ya jumamosi tarehe 3 mwezi may katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakili Kikwajuni Zanzibar. ikiwa na Nyimbo kumi.