Zenj FM
Zenj FM
22 April 2025, 5:24 pm

Na Mwandishi wetu.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Ayoub Mohd Mahmoud ameitaka jamii kupokea mabadiliko ya ongezeko la dozi ya chanjo ya polio kwa watoto ili kuwakinga na ugonjwa huo ambao husabaisha ulemavu au kufariki dunia .
Ameyasema hayo Afisi ya Mkoa Tunguu wakati akizungumza na Maafisa wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa, watendaji wa ofisi hiyo pamoja na viongozi wa idara ya chanjo na kinga kutoka wizara ya afya kwa lengo la kutoa elimu juu ya mabadiliko ya chanjo hiyo.
Amesema Tanzania ikiwemo Zanzibar ni miongoni mwa Nchi ambazo zimekua zikilipa umuhimu suala chanjo kwa wananchi wake hali ambayo imepelekea kuiwezesha nchi kuwa na idadi ndogo ya watu wanaoathirika na magonjwa mbali mbali ikiwemo ugonjwa huo ukilinganisha na baadhi ya nchi nyengine ulimwenguni hivyo ni vyema kwa wazazi kupeleka watoto wao wakati utakapowadia ili kuwakinga na mgonjwa.
Aidha amesema Serikali imekuwa makini na ina jali wananchi wake katika kuwakinga juu ya madhara ya magonjwa mbalimbali hivyo amewasisitiza wananchi kuondokana na dhana potofu kuwa chanjo hizo zina madhara na mabadala yake kuunga mkono juhudi za serikali katika kutokomeza magonjwa hatarishi nchini.
Nae Mkurugenzi huduma za kinga Zanzibar kutoka Wizara ya Afya Dkt Salim Slim amesema lengo la Serikali kupitia Wizara ya afya ya kutoa chanzo hizo ni kutokomeza kabisa ugonjwa huo kwa jamii hasa kwa watoto.
Nao washiriki wa kikao hicho wameahidi kuieneza elimu hiyo kwa jamii ili kuona zoezi hilo linafanikiwa kama ilivyokusudiwa.
zoezi hilo la chanjo ya polio ya kutumia njia ya sindano linalotarajiwa kufanyika tarehe 1 mei litahusisha watoto kuanzia umri wa miezi tisa katika maeneo yote ya unguja na pemba. mkoa