Zenj FM
Zenj FM
22 April 2025, 5:00 pm

Na Is-haka Mohammed
Chama cha Ada-Tadea kimewataka wananchi kutosikiliza maneno yanayotolewa na baadhi ya wana siasa yenye lengo la kuchafua amani na utulivu uliopo nchini bali waunge mkono juhudi za maendeleo zilizoletwa kwao na serikali.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa Chama cha Ada-Tadea Ali Makame Issa wakati akizungumza na wananchi alipokuwa akifungua Tawi la Chama hicho na kupokea wanachama wapya waliojiunga nacho wakitokea katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema huko katika kijiji cha maambani jimbo la kojani.
Amesema Serikali za Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamefanikiwa kufikisha maendeleo makubwa kwa wananchi katika maeneo mbali mbali ikiwemo katika jimbo la Kojani.
Aidha Mkurugenzi huyo amewataka wananchi hao kutokubaliana na viongozi wenye lengo la kutaka kuvunja muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa Kisingizio cha Mamlaka Kamili ya Zanzibar.
Akizungumzia kwa nini wameamua kukihama Chadema pamoja na kushusha bendera na kupandisha ya Ada-Tadea aliyekuwa Mwenyekiti wa jimbo la Kojani wa Chadema Moh`d Khamis Hamad amesema ni kutokana na kutokubaliana na kauli za viongozi wakuu wa chama hicho.
Zaidi ya Wanachama 21 waliokuwa wa Chadema katika jimbo la Kojani wamekihama cha hicho na kujiunga na Ada-Tadea.