Zenj FM

Halotel yakabidhi madawati skuli ya Kibweni

28 March 2025, 5:19 pm

Mkuu wa Kitengo cha Huduma na Bidhaa wa Halotel, Sakina Makabu, akimkabidhi Naibu Meya wa Wilaya ya Magharib A, Khadija Omar Ngarama, msaada wa madawati na vyakula kwa ajili ya skuli ya Kibweni,

Mary Julius.

Katika kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya nane katika sekta ya elimu, Halotel wamekabidhi madawati kwa skuli ya Kibweni.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo yaliyofanyika katika skuli ya Kibweni, iliyopo Mtoni, wilaya ya Magharib A, Naibu Meya wa Wilaya ya Magharib A, Khadija Omar Ngarama, ameupongeza Mtandao wa Halotel kwa kumsaidia Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa vitendo katika sekta ya elimu.
Khadija amesema msaada huo wa madawati utawasaidia wanafunzi kusoma kwa bidii na kwa uhuru, na hivyo kuchangia kupata ufaulu mzuri.
Aidha, amesema msaada huu ni hatua muhimu katika kuboresha mazingira ya kujifunzia, na kuhimiza maendeleo zaidi katika sekta ya elimu hivyo Naibu Meya amewaomba Halotel kuendelea kutoa msaada katika jimbo la Mtoni, hasa katika kuleta maendeleo katika shehia zote zilizopo kwenye jimbo hilo.

Sauti ya Naibu Meya wa Wilaya ya Magharib A, Khadija Omar Ngarama.

Akiitambulisha kampeni maalumu ya Marhaba Zanzibar, Mkuu wa Kitengo cha Huduma na Bidhaa wa Halotel, Sakina Makabu, amesema kampeni ya Marhaba Zanzibar ni maalum kwa Wazanzibar.
Aidha amesema Kampeni inakusudia kuwapa Wazanzibar ofa na huduma mbalimbali ambazo zitawasaidia katika nyanja za mawasiliano, na kuwa sehemu ya maendeleo ya jamii ya Zanzibar.

Sauti ya Mkuu wa Kitengo cha Huduma na Bidhaa wa Halotel, Sakina Makabu,

Naye Meneja wa Tawi la Halotel Zanzibar, Abubakar Adamu, amesema Halotel inaunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha elimu kwa kuwawezesha wanafunzi kupata vifurushi rahisi vya intaneti ili waweze kujifunza kupitia mitandao.
Amesema Halotel itaendelea kuisaidia serikali katika kuboresha miundombinu ya elimu ili kufikia malengo ya kutoa elimu bora kwa wananchi wa Zanzibar.

Sauti ya Meneja wa Tawi la Halotel Zanzibar, Abubakar Adamu.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Msingi Kibweni, Khadija Ali Suleiman, ameishukuru Halotel kwa kuiteua skuli hiyo na kufanya ufunguzi wa kampeni ya Marhaba Zanzibar, pamoja na kutoa msaada wa madawati ambao utawasaidia wanafunzi kusoma katika mazingira bora na yenye urahisi.
Aidha, Mwalimu Khadija amempongeza Mbunge wa Jimbo la Mtoni Abdulhafar Idrissa Juma kwa juhudi zake za kuwajengea madarasa katika shule hiyo amesema ujenzi wa madarasa hayo umechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha mazingira ya masomo na kuongeza ufanisi katika skuli hiyo.

Sauti ya Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Msingi Kibweni, Khadija Ali Suleiman.