Zenj FM

PharmAccess yachangia misingi imara ya huduma za afya kidijitali Zanzibar

26 March 2025, 4:48 pm

Waziri wa Afya Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui aliyevaa kanzu akiwa na viongozi wa wizara ya afya Zanzibar pamoja na Mkurugenzi Mkaazi wa PharmAcess katika hafla ya uhamasishaji wa matumizi ya kadi ya matibabu hafla ilifanyika katika ukumbi wa Golden Tulip Uwanja wa Ndege Mjini Unguja.

Na Mary Julius.

Waziri wa Afya Zanzibar,Nassor Ahmed Mazrui amewaomba wananchi, kuzitunza na kuzitumia kadi za matibabu kila wanapohitaji huduma za afya kwani kadi hizo ni nyenzo muhimu ya kuhakikisha huduma wanazopata zinaboreshwa na kuimarishwa kulingana na mahitaji halisi ya yaliyopo.

Akizungumza katika hafla ya uhamasishaji wa matumizi ya kadi ya matibabu hafla ambayo ilifanyika katika ukumbi wa Golden Tulip uwanja wa ndege Mjini Unguja ikiwa na lengo la kuinua mwamko wa jamii katika matumizi ya Kadi ya matibabu ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakiratibiwa na Shirika la PharmAcess ambapo kwa sasa wamekabidhi rasmi uratibu wa mpango huo kwa wizara ya afya.

Waziri ameishukuru PharmAcess kwa jitihada zilizopelekea ufanisi wa utekelezaji wa utaratibu wa mpango huu waziri ameahidi kuendeleza jitihada hizo kwa kutumia ujuzi na uzowefu uliojengwa kwa muda mrefu na Shirika la hilo.

Aidha waziri ameiomba Wizara ya Nchi Afisi ya Rais tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ kupitia kurugenzi ya Uratibu wa shughuli za SMZ kuunga mkono juhudi za kuhamasisha matumizi ya kadi za matibabu na kuwahamasisha viongozi katika ngazi za Shehia na Wilaya.

Amesema tangu kuanzishwa kwa mfumo huu mwaka 2020, wamefanikiwa kusajili zaidi ya ya wakaazi 1,739,391 wa Zanzibar, ikiwa ni 92% ya idadi ya watu wa Zanzibar ambapo mfumo huo umeunganishwa na mifumo mengine ya kielektroniki (EMRs) ya kurikodi taarifa za wagonjwa katika ngazi mbalimbali za utoaji wa huduma za Afya, kuanzia vituo vya afya vya msingi hadi hospitali za mikoa.
Aidha Amewataka wananchi kufuata taratibu na maelekezo yanayotolewa kuhusiana na matumizi ya kadi ya Matibabu ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa zinazokusanywa kupitia mfumo huo.

Sauti ya Waziri wa Afya Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui.
Mkurugenzi wa Mkaazi wa Taasisi ya PharmAccess, Heri Marwa, akimkabidhi mfano wa kadi ya matibabu Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mkaazi wa Taasisi ya PharmAccess, Heri Marwa, amesema pharmaAcess imeshirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji mzuri wa taarifa za afya ili kuhakikisha rasilimali zinazo tolewa na serikali kwa ajili ya kutoa huduma bora kwa wananchi zinatumika ipasavyo.
Aidha amesema mfumo huo utasaidia serikali kuwa na taarifa rasmi kwa huduma wanazotoa na kila senti inayotolewa inawafikia walengwa.

Sauti ya Mkurugenzi wa Mkaazi wa Taasisi ya PharmAccess, Heri Marwa.

Akielezea faida ya kadi hizo Mkurugenzi Mipango Sera na Utafiti Wizara ya Afya Abdullatif Khatibu Haji amesema mfumo huo wa kutumia kadi ya matibabu utaisaidia wizara ya afya kupata taarifa sahihi ambazo itasaidia kufanya maamuzi sahihi katika kupanga bajeti ya wizara hiyo.
Aidha amesema matumizi ya kadi hizo yatasaidia kufuatilia vyanzo vya maradhi katika jamii hali ambayo itasaidia kuwatambua wagonjwa mapema na kuweza kuchukua hatua za haraka pamoja na kusaidia kupima hali ya umaskini katika jamii.

Sauti ya Mkurugenzi Mipango Sera na Utafiti Wizara ya Afya Abdullatif Khatibu Haji.

Tangu kuanzishwa kwa mradi huu mafanikio makubwa yamepatikana kupitia utaratibu wa kadi za Matibabu ambapo kila mgonjwa aliyesajiliwa hutambuliwa kwa kutumia Kadi ya Matibabu katika vituo vya Afya,hatua hii imerahisisha utoaji wa huduma kwa haraka na ufanisi zaidi ambapo kwa kutumia kadi hii ni rahisi kujua idadi halisi ya watu wanaopata huduma katika hospitali , hasa za wilaya na mikoa.