Zenj FM

Pemba waomba ligi ya mpira wa pete

25 March 2025, 2:56 pm

Wachezaji wa Timu ya timu ya Netball ya Mchanga mdogo Center wakiwa na maofisa wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar(TAMWA) huko katika uwanja wao wa mazoezi huko Skuli ya Mchanga mdogo msingi.

Na Is-haka Mohamed

Kutokuwepo kwa mashindano ya aina mbalimbali kunaelezwa kuhatarisha kutoweka kabisa kwa mpira wa pete (Netball) kisiwani Pemba.

Hayo yameelezwa na baadhi ya wachezaji wa mpira huo katika timu ya Mchangamdogo Centre wakati walipotembelewa na timu ya waandishi wa habari za michezo kujua maendeleo yao huko katika uwanja wao wa mazoezi Skuli ya Mchangamdogo msingi.

Wakizungumzia changamoto hiyo mchezaji Amina na Zainab wa timu ya Mchangamdogo Centre wamesema kuwa kutokuwepo kwa mashindano kunawadumaza na kukiomba Chama cha mchezo huo kutanua mbawa ili ligi ya mchezo huo ifanyike Pemba.

Sauti za wachezaji Amina na Zainab.

Bimkubwa Maulid Othman ni Katibu wa timu ya Mpira wa Pete ya Wanawake ya Mchanga Mdogo Centre amesema kuwa kukosekana kwa mashindano wamekuwa wakiishia kwenye mabonaza yasiyo Rasmi jambo ambalo amesema halina afya njema kwa maendeleo ya mchezo huo Pemba.

Sauti ya Katibu wa timu ya Mpira wa Pete ya Wanawake ya Mchanga Mdogo Centre Bimkubwa Maulid Othman

Akizungumzia changamoto hizo Makamo Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Pete Wilaya ya Wete Idrissa Maulid Othman amekiri kuwa hadi sasa kwa kisiwani Pemba hakuna mashindano Rasmi ya Mpira huo.

Sauti ya Makamo Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Pete Wilaya ya Wete Idrissa Maulid Othman.

Hata hivyo Afisa wa Mawasiliano wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar Khairat Haji Ali amesema juhudi zao za kuhamasisha wanawake kushiriki kwenye michezo kupitia mradi wa Michezo kwa Maendeleo zimeonekana kuanza kupata mafanikio japo bado kuna changamoto nyingi.

Sauti ya Afisa wa Mawasiliano wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar Khairat Haji Ali.

Katika miaka ya 1960- 1980 timu za Zanzibar za mpira wa Pete ambapo kwa wakati huzo ukichezwa sana na wanawake zilikuwa ni miongoni mwa timu tishio katika ukanda huu wa Afrika ya Mashariki na Kati, kwani ziliweza kufanya vizuri katika mashindano mbali mbali yakiwemo yale ya vilabu na timu za taifa.