

7 March 2025, 5:41 pm
Na Is-haka Mohammed.
Waendesha Bajaji wa Wilaya ya Chake Chake Pemba wamesema faini wanazootozwa mara kwa mara na mamlaka za serikali ikiwemo mamlaka ya usafiri kupitia Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Pemba umekuwa ukirejesha nyuma kazi zao hizo.
Wakizungumza juu ya faini hizo na madhara yake kwao baadhi ya waendesha bajaji katika Mkoa wa Kusini Pemba huko Tibirinzi Chake Chake wamesema faini hizo ni adhabu inayopelekea kufanya kazi zao kwa hasara.
Wamesema watendaji wa Mamlaka ya Usifiri wamekuwa wakitoa adhabu kubwa kwa makos ahata madogo yasiyoendana na uhalisia wa kiwango cha fedha wanachotozwa.
Aidha waendesha Bajaji hao wametoa wito kwa uongozi wa Wizara kufuatilia malalamiko yao na kuyafanyia kazi kwani lengo la serikali ni kuwawezesha vijana kujiajiri kupitia njia hiyo na sio kuwanyanyasa.
Akizungumzia juu ya malalamiko ya Waendesha Bajaji Mkoa wa Kusini Pemba Mkaguzi wa Mawasiliano Pemba Hamad Salim Hamad amesema njia bora ya kuepuka adhabu na faini kwa waendeshaji bajaji hao ni kufuata sheria wanapokuwa barabarani.
Maulid Mwalim Khamis ni Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Chake Chake amewataka waendesha Bajaji kushirikiana na mamlaka za serikali zinazowasimamia ili kuona kuwa changamoto zao zinapatiwa ufumbuzi.
Mapema Mwenyekiti wa Jumuiya ya Waendesha Bajaji na Bodaboda Mkoa wa Kusini Pemba Moh`d Kassim Idd ameiomba Serikali kuangalia kwa makini suala la faini wanazotoza kwa Bajaji kwani ni kubwa sana.
Kikao hicho kilichofanyika uwanja wa Mpira Tibirinzi kiliathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za usafiri kwa abiria wanaotumia usafiri huo kutokana na waendesha bajaji na bajaji zao kuhudhuria kikao hicho.