

27 February 2025, 3:28 pm
Na Mary Julius.
Mwakilishi Viti Maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM anayewakilisha kundi la watu wenye ulemavu Mwantatu Mbaraka Khamisi amewataka viongozi watakaochaguliwa kuongoza Umoja wa Watu Wenye Ulemavu (UWZ) kujitolea kwa hali na mali ili kuhakikisha umoja huo unaendelea na kufikia malengo waliojiwekea.
Mwakilishi mwantatu ameyasema hayo Katika ufunguzi wa mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Umoja huo uliofanyika katika ukumbi wa UWZ, Kikwajuni Zanzibar, Mwamtatu amesema maendeleo ya umoja huo yanahitaji juhudi za pamoja, ushirikiano, na uvumilivu kutoka kwa viongozi,watakao chaguliwa na wanachama kwa ujumla .
Mwantatu ametoa pongezi kwa viongozi wa Umoja wa Watu Wenye Ulemavu kwa juhudi zao za kuhakikisha umoja huo unasimamia demokrasia katika upatikanaji wa viongozi. Pia, amewataka kuendeleza umoja na mshikamano katika kipindi cha uchaguzi, na kuwataka wanachama wa umoja huo kuhakikisha kuwa uchaguzi hautaleta migawanyiko au makundi ambayo yanaweza kuathiri umoja huo.
Aidha, Mwamtatu amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, dk Husein Ali Mwinyi kwa kuhakikisha miundombinu inayojengwa inazingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu, jambo ambalo limesaidia kuboresha maisha ya kundi hilo.
Akimkaribisha mgeni Rasmi Mwenyekiti Mstaafu wa Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar Salma Haji Sadat amesema umoja huo umeleta mafanikio makubwa kwa watu wenye ulemavu kwa upande wa Zanzibar. Aidha Mwenyekiti ameiomba serikali ya mapinduzi ya Zanzibar kuziangalia barabara za ndani kwani miundo mbinu yake sio rafiki kwa watu wenye ulemavu.
Kwa upande wake,Mwenyekiti Mpya wa Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar Abdulwakili H Hafidhi amesema katika kukabiliana na uhaba wa wafadhili katika umoja huo ameyaomba mashirika na watu wenye uwezo wa kifedha nchini kuchukua jukumu la kusaidia na kuwa na mchango wa kudumu katika kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu, badala ya kutegemea misaada ya wafadhili peke yake .
Abdulwakili amesema misaada kutoka kwa mashirika na watu wenyeuwezo unaweza kusaidia kujaza pengo la kifedha linalojitok kutokea kutokana na kutegemea wafadhili katika kuendesha umoja huo.
Aidha, Mwenyekiti Abdulwakili, amewataka wanachama wa umoja huo kuungana na kushirikiana kwa ukaribu ili kuweza kuendeleza umoja na kufikia malengo yao. Amesisitiza kuwa umoja na ushirikiano ni muhimu katika kuhakikisha kuwa changamoto zinazokabili watu wenye ulemavu zinatatuliwa kwa pamoja.
Katika mkutano huo viongozi mbalimbali walichaguliwa na Mkutano wa Mkuu wa Uchaguzi wa Umoja wa Watu Wenye Ulemavu ambapo umemchaguwa Mwenyekiti Abdulwakili H Hafidhi Makamo Mwenyekiti aliyechaguliwa ni Haji Khamis Nyange kwa nafasi ya Katibu Mkuu aliyechaguliwa ni Yahya Hemed Said, na kwa upande wamshika fedha Mkutano Mkuu umemchagua Anas Rashid Ramadhani.