Zenj FM

Afisa Elimu Wilaya ya Kati atoa wito wazazi kuandikisha watoto skuli

6 January 2025, 3:02 pm

Afisa Elimu Wilaya ya Kati Somoe Said Mussa akizungumza na Masheha wa Shehia 42 za Wilaya ya Kati, Waratibu wa Wanawake na Watoto, Wawakikishi wa Mabaraza ya Vijana na Makatibu wa Kamati za Skuli za Maandalizi na Msingi Kwa Wilaya ya Kati.

Na Mary Julius.

Afisa Elimu Wilaya ya Kati, Somoe Said Mussa, ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanawaandikisha watoto wao waliotimia umri wa kuanza skuli ili waweze kupata haki yao ya msingi, ambayo ni elimu.

Kauli hiyo ameitoa alipokuwa akitoa mafunzo ya uhamasishaji kuhusu uandikishaji wa wanafunzi wapya wa skuli za maandalizi na msingi.

Mafunzo hayo ambaayo yamelenga kuwafikia wazazi kupitia masheha, waratibu wa wanawake na watoto, mabaraza ya vijana, na makatibu wa kamati za shule huko TC Dunga, Wilaya ya Kati Unguja.

Katika mafunzo hayo, Somoe amesisitiza kuwa kila mtoto anapaswa kupewa elimu bora itakayomuwezesha kufikia malengo aliyojiwekea.

Aidha amesema ni jukumu la wazazi kuhakikisha watoto wao wanapata elimu bora, kwani hiyo itawapa fursa ya kujitambua na kufikia mafanikio maishani.

Sauti ya Afisa Elimu Wilaya ya Kati, Somoe Said Mussa,

Naye Mratibu wa Wanawake na Watoto Shehiya ya Kikungwi, Bahati Issa Suleiman, ameishukuru serikali kwa jitihada zake katika kulikazia suala la elimu na kutambua umuhimu wa watoto kupata elimu bora.

Amesema serikali imeonyesha kujali na kutoa kipaumbele katika kuhakikisha kwamba watoto wa jamii wanapata fursa ya kupata elimu ya kiwango cha juu, jambo ambalo litawafaidi katika kujenga mustakabali wao.

Sauti ya Mratibu wa Wanawake na Watoto Shehiya ya Kikungwi, Bahati Issa Suleiman.

Nae Sheha wa Shehia ya Jendele Zidi Suleiman amesema  watahakikisha wanatoa elimu  nyumba hadi nyumba ili kuiona jamii inapata uelewa na mwamko wa kuwaandikisha watoto wao kwa ajili ya elimu.

Sauti ya Sheha wa Shehia ya Jendele Zidi Suleiman.