Uzinduzi wa Tawi la TAWEN Zanzibar Utaongeza Fursa za Kiuchumi kwa Wanawake
29 December 2024, 4:13 pm
Na Mary Julius.
Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Mgeni Hassan Juma amesema kuzinduliwa kwa tawi la Taasisi ya Tanzania Women Enpowerment Network Zanzibar TAWEN kutawezesha wanawake kuzifikia fursa za kiuchumi zinazo tolewa na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Naibu spika Mgeni ameyasema hayo katika uzinduzi wa Tasisi ya Tanzania Women Empowerment Network Tawi la Zanzibar hafla iliyo fanyika Mazizini, amesema Uzinduzi huu unalenga kuwakomboa wanawake kwa kuwapa fursa mbalimbali za kiuchumi zinazotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwa na lengo la kuwawezesha wanawake kufikia na kutumia fursa hizo ili kuboresha maisha yao na kuchangia katika maendeleo ya uchumi wa Zanzibar.
Aidha Ameipongeza TAWEN kwa kuokoa maisha ya wanawake na vijana kwa kuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu na msaada kwa jamii, hasa wanawake na vijana, kuhusu faida za kutumia nishati safi kama vile gesi, jiko la mkaa wa kisasa, na pia inachangia katika kulinda mazingira kwa kupunguza ukataji wa miti na uchafuzi wa mazingira.
Kwa upande wake Mkurugenzi Taasisi ya Tanzania Women Empowerment Network (TAWEN), Florence Masunga amesema lengo kuu la Taasisi hiyo ni kuwasaidia wanawake katika masuala mbalimbali ya kiuchumi ili waweze kupiga hatua za kimaendeleo.
Akizungumza katika uzinduzi huo Mlezi wa Taasisi ya TAWEN Amina Salum Ali amesema kwa upande wa Zanzibar nyumba nyingi zinaongozwa na wanawake hivyo kuwa na jukumu kubwa katika familia na jamii.
Aidha amesema kwa kushirikiana na serikali taasisi hiyo itawasaidia wanawake katika kujikomboa kiuchumi na kuhakikisha wanatumia nishati salama ya kupikia.
Nae Makamo mwenyekiti wa TAWEN Thuweiba Edington Kisasi amesema jukumu la TAWEN ni kushikana mkono na wanawake na vijana ili kuweza kuimarisha maendeleo yao.
Mrajis wa NGOs Zanzibar Ahmed Khalid Abdulla ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha tawen inapiga hatua ili kuhakikisha TAWEN inafikia malengo yake.
Kuzinduliwa kwa tawi la Zanzibar linaifanya taasisi ya TAWEN kuwa na matawi kumi na moja Tanzania ikiwa na kauli mbiu ya ni Wakati wa Mwanamke ni Sasa Inuka. kijana: Nafikiaje Ndoto yangu?