SMZ na mafanikio katika sekta ya elimu Jimbo la Malindi
10 December 2024, 6:38 pm
Na Mary Julius.
Mwakilishi wa Jimbo la Malindi Mohamed Ahmada Salum amesema mazingira mazuri ya elimu yaliyowekwa na serikali ya awamu ya nane yamesaidia kuboresha matokeo katika mitihani ya taifa.
Ahmada ameyasema hayo katika hafla ya kuwapongeza wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani yao ya wa kidato cha nne na sita pamoja na kuwaaga walimu 4 waliostaafu katika skuli ya kiponda halfa iliyofanyika Jambiani, Mkoa wa kusini unguja.
Amesema juhudi za Serikali katika kuboresha miundombinu ya skuli, kuongeza vifaa vya kisasa vya kujifunzia, na kutoa motisha kwa walimu na wanafunzi zimekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha viwango vya elimu na ufaulu wa wanafunzi.
Aidha amewapongeza walimu na wanafunzi wa Skuli ya Kiponda kwa kufanya vizuri katika mitihani hiyo ya taifa na kuwataka wanafunzi kuendeleza yale mazuri walio jifunza.
Akizungumzia walimu wastaafu Ahamada amewataka walimu hao kuwa waadilifu katika kutumia kinua mgongo.
Akizungumza katika hafla hiyo Afisa Elimu Wilaya ya Mjini Taaluma Wahida Haidar Khasham amewataka wanafunzi hao kuendeleza mafunzo yale yote waliyopewa na walimu pamoja na wazazi na kuwataka kuto kukata tamaa katika kuitafuta elimu.
Akizungumza kwa niaba ya walimu wastaafu Mwalimu Saidi Abubakari amewataka walimu kuifanya kazi kwa bidii na kujitoa ili kujenga elimu kwa watoto.
Kwa upande wao wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani yao wamewapongeza walimu kwa kufanya bidii katika kuwafundisha na kuwataka wanafunzi kuzitumia changamoto zao katika kuongeza bidii katika masomo yao ili waweze kupata matokeo mazuri.