Dk Mwinyi ahimiza jamii kufanya mazoezi Zanzibar
8 December 2024, 4:59 pm
Na Mary Julius.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuchukua juhudi maalum kuhakikisha inapunguza kasi ya ongezeko la Maradhi yasiombukiza nchini.
Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo alipozungumza baada ya Kuongoza matembezi ya Afya yalioandaliwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Taasisi ya Pharm Access ikiwa ni kampeni maalum ya kudhibiti Maradhi yasioambukiza kwa jamii yalioanzia Kiembe Samaki kwa Boutros hadi Uwanja Mao Tse Tung Wilaya ya Mjini.
Rais Dk.Mwinyi amesema Takwimu za Wizara ya Afya zimeeleza kuwa kuna Ongezeko la Maradhi Yasioambukiza kwa kiwango kikubwa ikwemo Kisukari, Presha , Uzito na Unene uliopitiliza na shinikizo la damu kunakosababishwa na watu wengi kutofanya mazoezi.
Aidha Rais Dk.Mwinyi ametoa wito kwa kila mmoja kuchukua hatua ya kupunguza matumizi ya vyakula vya wanga na mafuta ili kukabiliana na maradhi hayo.
Nae Waziri wa Afya Zaznibar Nassor Ahmed Mazrui amesema Dhamira ya Serikali ni kuona wananchi wote wana afya njema na kutambua kuwa suala la kufanya mazoezi sio anasa na Wizara inajiandaa kuwa na siku maalum ya mazoezi kila mwezi.
Aidha Ametoa rai kwa Taasisi za Umma na binafsi kuandaa utaratibu wa kuwa na siku maalum ya kufanya mazoezi.
Akizungumza mara baada ya matembezi hayo Mkurugenzi Mtendaji Pharm Access Dk Heri Marwa amesema lengo la matembezi hayo ni kuihamasisha jamii kufanya mazoezi ili kuepukana na maradhi yasioambukiza.
Mkurugenzi Marwa amesema tatizo la magojwa yasio ambukizwa limekuwa janga kubwa duniani na kuitaka jamii kuachana na dhana potofu ya kuwa magojwa yasioambukizwa ni ya matajiri tu na badala yake kuchukua hatua katika kupambana na maradhi hayo.
Kwa pande wake Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dkt Mngereza Mzee Miraji amesema sekta ya afya Zanzibar inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya ongezeko la maradhi yasioambukiza.
Matembezi ya afya yamebeba kaulimbiu inayosema “chagua mazoezi kuwa sehemu ya maisha”