Zenj FM

UWZ yawafikia watu wenye ulemavu kisiwa cha Kojani

4 December 2024, 9:39 pm

Mkurugenzi wa Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar (UWZ) Asia Abdulsalam Hussein akikabidhi msaada kwa mtoto wenye ulemavu Kojani,

Na Mary Julius.

Mkurugenzi wa Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar Asia Abdulsalam Hussein ameiomba jamii  kuwasaidia watu wenye ulemavu, hasa wale wanaoishi katika visiwa vidogo vidogo vilivyopo Zanzibar.

Mkurugenzi Asia ameyasema hayo mara baada ya ziara ya kuwatembelea watu wenye ulemavu katika kisiwa cha Kojani Pemba na kugawa misaada mbalimbali kwa watu wenye ulemavu na wasio na ulemavu katika kisiwa hicho, amesema watu wanaoishi katika visiwa kama cha Kojani amesema watu wenye ulemavu katika maeneo haya wanakutana na changamoto kubwa ya kupata huduma muhimu za kijamii, kama vile elimu, afya na usafiri.

Aidha Mkurugenzi amesema msaada kutoka kwa jamii, serikalini na mashirika ya kiraia utaleta mabadiliko makubwa kwa watu wenye ulemavu, kuhakikisha wanapata fursa sawa katika jamii na kupunguza ubaguzi dhidi yao.

Mkurugenzi wa Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar Asia Abdulsalam Hussein akikabidhi msaada,

Kwa upande mwingine Mkurugenzi Asia amesema watu wenye ulemavu wanahitaji lishe bora ili waweze kuwa na nguvu na afya njema, lakini kwa bahati mbaya, wengi wao wanakosa chakula cha kutosha na cha virutubisho muhimu.

Lishe duni kwa watu wenye ulemavu kisiwa cha Kojani inaathiri uwezo wao wa kukabiliana na changamoto za kimwili na kiakili, na inaweza kuongeza hatari ya kupata magonjwa mbalimbali.

Aidha, Mkurugenzi ametoa wito kwa taasisi za afya, mashirika ya kiraia na jamii kwa ujumla kuchukua hatua za haraka ili kuboresha hali ya lishe kwa watu wenye ulemavu, hasa katika maeneo ya vijijini na visiwa vidogo vidogo.

Sauti ya Mkurugenzi wa Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar Asia Abdulsalam Hussein.

Kwa upande wake Sheha wa Kojani Hamad Ali Bakame amesema amefurahishwa na msaada uliotolewa na umoja huo kwa watu wenye ulemavu wa kojani kitendo hicho kimewapa faraja.

Sauti ya Sheha wa Kojani Hamad Ali Bakame.

Nao Wazazi wenye watoto wenye ulemavu wameushukuru Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar kwa kuwapatia misaada itakayo wasaidia katika malezi ya watoto wao.

Wazazi hao wamesema familia nyingi zinazolea watoto wenye ulemavu zinakutana na changamoto kubwa za kifedha na kijamii, na msaada huo  umekuwa ni mkombozi kwao.

Aidha, wazazi wametoa wito kwa jamii na serikali kuendelea kushirikiana na Umoja wa Watu Wenye Ulemavu ili kuhakikisha msaada zaidi unaendelea kuwafikia watoto wenye ulemavu.

Sauti ya wazazi.
Wafanyakazi wa Umoja wa Watu wenye Uemavu wakiwa katika kivuko kuelekea Kisiwa cha Kojani.

Zaidi ya watu miambili walio na ulemavu na wasio na ulemavu wamepokea msaada huo,ikiwa ni katika kuadhimisha siku ya Watu Wenye Ulemavu ambapo kwa Zanzibar  siku hiyo imeadhimishwa kisiwani Pemba  Mkoa wa Kusini Pemba.

Misaada iliyotolewa ni Sabuni za kufulia, unga wa lishe, nguo, pempasi, biskuti na soda.