Wanahabari Pemba waaswa kuandika habari za kuinua sauti za wanawake
6 November 2024, 5:15 pm
Na Is-haka Mohammed.
Waandishi wa Habari kisiwani Pemba wameaswa juu kuandika Habari zitakazosaidia kuwezesha kusikiika kwa sauti za wanawake zinazohusu mabadiliko ya tabia ya nchi na athari zake, ili sauti za wanawake hao zipate kusikika na kuondokana na changamoto zinazojitokeza za kupata haki zao za kutosikika.
Mjumbe wa Bodi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tamwa-Zanzibar Mwatima Rashid Issa ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wanaoshiriki katika mafunzo maalum ya yanayohusiana na mabadilo ya tabia nchi na athari zake hasa kwa wanawake na watoto yaliyofanyika katika ukumbi wa ofisi ndogo za Tamwa zilizopo Mkanjuni Chake Chake.
Amesema Tamwa Zanzibar imebaini kuwepo kwa changamoto kubwa kwa waandishi wa habari kisiwani Pemba katika kupaza sauti za wanawake wanaokabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabia ya nchi jambo ambalo hurejesha nyuma wanawake hao katika harakati zao.
Akiwasilisha mada kwa waandishi wa habari Mwandishi wa Mwandamizi anayeongoza mafunzo hayo ya Zan-Adapt, Ali Mbraouk Omar amesema shughuli za kiasili zinazofanywa na binaadmu ikiwemo kukata miti, uvuvi haramu, kuongezeka joto na nyenginezo hupelekea kuleta athari kwa akina mama na wanawake katika shughuli zao.
Awali akielezea mradi huo Afisa mawasiliano wa Tamwa Zanzibar Nafda Hindi Moh`d amesema kuwa lengo la mradi huo ni kuona waandishi wa habari visiwani hapa wanaandika habari zinazomnyanyua mwanamke katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi na katika uongozi.
Nao baadhi ya waandishi wa Habari akiwemo Habiba Zarali Rukuni na Abdi Juma Suleiman wamesema mafunzo hayo yatawasaidia kubadilisha mitazamo yao katika kuandika Habari zinazowahusu wanawake na mabadiliko ya tabia ya nchi.
Mafunzo hayo ya siku 2 yanayotolewa kwa waandishi wa habari 30,ikiwa 20 ni kutoka Kisiwani Unguja na 10 Pemba ni utekelezaji wa mradi wa Zanz- Adopt unaotekelezwa kwa mashirikiano kati ya Tamwa, Community Forest Pemba na Community forest International kwa ufadhili wa Canada.