Majengo ya Mjerumani yazusha mzozo Zanzibar
3 November 2024, 3:18 pm
Na Mwandishi wetu
Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC) limetangaza kuwaondoa na kuwahamisha wakaazi wanaoshi kwenye majengo yaliojengwa na iliokuwa serikali ya ujerumani mashariki Zanzibar kwa miaka sitini sasa kwa madai ya kutaka kuvunjwa ili kupisha uwekezaji mpya. .
Mgogoro umezuka na kuwaibua watu kadhaa akiwemo mtoto wa pili wa Rais wa kwanza Zanzibar Balozi Ali Abeid Karume pamoja na mbunge wa zamani jimbo la Kikwajuni Parmukh Hogan Sigh.
Balozi Karume amesema uamuzi wowote wa kuvunja majengo hayo na wananchi kuhamishwa kwa nguvu, kunaweza kuleta mtafaruku kati ya SMZ na wananchi.
Balozi Karume amedai yupo mtu ambaye kwa dhamira mbaya anafikiri anataka kuleta ukorofi ili kuvuruga nia njema ya serikali ya CCM huku akichochea uvunjifu wa umoja na amani .
Amesema ni vema Shirika la Nyumba Zanzibar likaelewa sababu za ujenzi wa nyumba hizo,kwanini zilijengwa ,nani mjenzi wake na zimeachwa chini ya dhamana ipi baada ya kumalizika kuliko kufanya watakavyo.
Naye Mbunge wa zamani wa kikwajuni Parmukh Singh Hogan amesema kuvunjwa nyumba hizo ni mwanzo wa kufutwa kwa historia kati ya ujerumani na Zanzibar pia kwa Jamhuri ya Muungano sababu wao ndiyo waliojenga baada ya Mapinduzi.
Ujerumani Mashariki ndio taifa la kwanza duniani kuyatambua Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964 ikafuatia China,baadae Cuba yakafuata mataifa mengine mengine duniani .
Sigh amesema ni busara endapo ujerumani itashirikishwa kwani hata aliookuja kiongozi wake kutembelea Zanzibar, alifika kuona majengo hayo hivyo haitakuwa sahihi kudhoofisha mahusiano ya taifa na taifa .
Kwa upande mwingine Mwenyekiti wa kamati ya kufuatilia mgogoro huo Jaha Ame Rajab ,amesema tayari wananchi wakaazi wa eneo hilo wameshaanza vikao vya kujadili suala hilo na viongozi wa SMZ .
Jaha amesema mkuu wa wilaya ya mjini Rashid Masaraka ameshakutana na kamati yake hivyo kuna mfululizo wa vikao vinavyoendelea lakini akasema bado haijajulikana hatma ya jambo hilo .
Amesema mahali hapo wanaishi watu toka awamu ya utawala wa kwanza wa SMZ hivyo uamuzi wowote wa kuwafukuza, unaweza kuamsha chuki,hamaki na mzozo mkubwa usiokwisha.
Nacho Chama cha ACT wazalendo kimesema uwamuzi wa huo ni kinyume na haki za binadamu lakini pia unapuuzia malengo ya Rais wa kwanza Abedi Amani Karume ya kuwapatia makaazi bora wananchi.
Waziri kivuli wa ardhi ACT Wazalendo…Rashid Ali Abdalla..amesema ingekuwa busara sana iwapo wananchi watashirikishwa na kutoa maoni yao kabla ya kupitishwa maamuzi mengine.
Nyumba za maghorofa Kikwajuni zilijegwa baada ya mapinduzi kama msaada wa kuwapatia makaazi bora wananchi na serikali ya ujerumani Mashariki.