Saratani ya shingo ya kizazi tishio Zanzibar
22 October 2024, 5:21 pm
Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mgeni Hassan Juma amesifu jitihada za Serikali ya watu China katika kuisaidia Zanzibar kwa nyanja tofauti ikiwemo sekta ya Afya hasa katika masuala mazima ya kupambana na maradhi ya saratani.
Kauli hiyo ameitoa katika Hospitali ya Wilaya Ijitimai wakati alipofanya uzinduzi wa uchunguzi wa maradhi ya saratani ya shingo ya kizazi yanayofanywa na madaktari kutoka China kupitia taasisi ya Jasmine- CLOVE ya Jiangsu nchini China kwa kushirikiana na Wizara ya Afya.
Amesema tangu kuanza kwa uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi hapa Zanzibar mafanikio makubwa yameweza kupatikana ikiwemo madaktari hao kuwafanyia matibabu ambao wamebainika na maradhi hayo sambamba na wataalamu wa hapa nchini kupata ujuzi wa kukabiliana na maradhi hayo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dkt Amour Suleiman Mohamed amesema kuwa kwa upande wa Zanzibar tatizo la saratani ya shingo kizazi ni kubwa sana ukilinganisha na maeneo mengine ya duniani na linachangia kwa kiasi kikubwa nguvu kazi wa uchumi wa nchi.
Aidha amesema kuwa gharama za tiba ya maradhi ya saratani ni ghali sana na uchumi wa kawaida hushindwa kumudu kujigharamia na Serikali hulazimika kugharamia matibabu ya wagonjwa hao kwa kuwapeleka Tanzania bara mara nyengine nnje ya nchi ambapo kwa mwaka wanapelekwa wagonjwa karibu hamsini hadi sitini na kwa mwezi zinalipwa milioni 50 hadi 60.
Nae Kaimu Balozi mdogo wa China Zanzibar Zhang Ming na mwakilishi kutoka taasisi ya clove wamesema wataendelea kukuza ushirikiano uliopo kati za Zanzibar na China katika kuimarisha huduma za afya na huduma nyengine hapa nchini hasa katika masuala mazima ya kupambana na saratani ya shingo ya kizazi.
Wanawake wenye umri kuanzia miaka 18 hadi 69 watafanyiwa uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi na kupatiwa matibabu kwa wale ambao watabainika na maradhi hayo huku uchunguzi huo ni wamara ya saba unaotolewa na madaktari kutoka china.