ZAECA yawafikia Madiwani Wilaya ya Kati
18 October 2024, 4:28 pm
Na Mary Julius.
Mkuu wa Idara ya Rasilimali watu Mipango na Utawala, Ofisi ya Baraza la Mji Kati Rehema Khamis Hassan, amewataka Madiwani kufuata Sheria na kutoa Elimu dhidi ya Rushwa na Uhujumu uchumi katika Wadi zao.
Rehema ametoa wito huo katika mafunzo ya utoaji wa Elimu kuhusiana na Rushwa na Uhujumu uchumi kwa Madiwani na Watendaji wa Wilaya ya Kati Unguja, amesema lengo la mafunzo hayo kwa madiwani hao ni kuwajulisha juu ya sheria na taratibu za kimsingi za uhujumu wa uchumi na rushwa.
Aidha Rehema amesema mafunzo hayo yatawawezesha madiwani kujua nini cha kufanya wanapo ona ishara za uhujumu uchumi katika miradi ya maendeleo iliyopo katika wadi zao.
Nae, Afisa Elimu kutoka Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu uchumi Zanzibar (ZAECA) Yussuf Juma, amewataka Madiwani kuhakikisha kua wanasimamia Sheria na taratibu katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Aidha amesema ni jukumu la Madiwani kuhakikisha wanaunga mkono Juhudi za Serikali katika kupambana na Vitendo vya Rushwa na Uhujumu uchumi, pamoja na kulinda Rasilimali za Nchi kwa kutoa taarifa katika Vyombo husika.
Kwa upande wake Diwani wa Wadi ya Ubago Ussi Ali Mtumwa, ambaye pia ni Makamo Mwenyekiti Baraza la Mji Kati, kwa niaba ya Madiwani wenzake amesema wamefarajika kwa kupatiwa mafunzo hayo, ambayo yatawawezesha kubadilika katika utendaji wao wa kazi, pamoja na kuisaidi Serikali katika kuimarisha Miradi ya Maendeleo.