Manispaa Magharibi “A” yajivunia Ongezeko la Mapato
11 October 2024, 5:34 pm
Na Mary Julius.
Ujenzi wa Kituo cha Mndo umefikia 76% ambapo kituo hicho kinatarajiwa kugharimu zaidi ya Millioni Mia Tisa hadi kukamilika kwake.
Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar imeahidi kumaliza ujenzi wa kituo cha dalala za abiria cha Mndo kwa kukiwekea lami ili kiweze kutoa huduma kwa wananchi.
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Dkt. Khalid Salum Mohamed ametoa ahadi hiyo katika sherehe za maadhimisho za kutimia miaka nane tokea kuanzishwa kwa Baraza la Manispaa Magharibi “A” sherehe zilizokwenda sambamba na uwekaji wa jiwe la msingi la kituo cha abiria cha MNDO.
Waziri Dkt. Khalid amesema kukamilika kwa kituo hicho kutachochea harakati za ukuaji wa uchumi kitendo ambacho kitasaidia kuwaingizia kipato wananchi mmoja mmoja kutokana na biashara watakazozifanya.
Aidha, Waziri amewataka watendaji wa baraza la Manispaa Magharibi “A” kuongeza kasi ya utendaji kazi na kuachana na farka, ugomvi, majungu na fitana kwani masuala hayo yanarudisha nyuma masuala ya kimaendeleo.
Nae, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Magharibi “A” ambae pia ni Mkuu wa Wilaya ya Magharib “B” Hamida Mussa Khamis amemuomba Waziri ujenzi wa barabara ya Kizimbani-Miwani uwende sambamba na hatua ya uwekaji wa lami katika kituo cha Mndo ili kuipendezesha mandhari ya eneo hilo.
Hamida amepongeza jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi za kuimarisha miundombinu nchini sambamba na kupongeza usimamizi mzuri wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi.
Akitoa maelezo ya kitaalamu Mkurugenzi wa Manispaa Magharibi “A” Mbaraka Said Hasuni amesema katika kipindi hichi cha kusherehekea kutimia miaka nane kuanzishwa Baraza la Manispaa Magharibi “A” limefanikiwa kuongeza mapato yake jambo linalosaidia kuimarika kwa huduma za jamii.
Mkurugenzi Mbaraka Hasuni amesema katika fedha hizo Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ itatoa shilling Millioni Mia Sita na zaidi ya Shillingi Millioni Mia Tatu zitatolea na Baraza la Manispaa Magharibi “A”.