Diwani Viti Maalum akagua miradi ya maendeleo Wilaya ya Kati
7 October 2024, 4:51 pm
Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii Baraza la Mji Kati ambaye pia ni Diwani wa viti maalum Riziki Muhammed Abdalla amewataka Wanajamii kushirikiana pamoja kuitunza na kuimarisha Miradi ya maendeleo inayojengwa katika maeneo yao ili iweze kudumu.
Riziki ameyasema hayo wakati alipo shiriki katika ziara ya ukaguzi wa maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Kati Unguja, Amesema lengo la kukagua Miradi hiyo ni kujiridhisha kutokana na yale ambayo yanawasilishwa katika Kamati za utekelezaji na uhalisia uliopo katika jamii.
Kwa upande wake Mkuu wa Divisheni ya Huduma za Jamii Baraza la Mji Kati Mussa Abdul-rabi Fadhil amesema Kamati imeridhishwa na utendaji kazi wa Wahandisi wa ujenzi wa miradi hiyo ambayo kwasasa inaendelea vizuri.
Aidha amewataka Wananchi kushirikiana kutoa taarifa kwa Vyombo husika kwa wale wote watakao husika kufanya uharibufu wa miradi hiyo,pamoja na kuwataka kuitunza miradi hiyo kwa lengo la kuweka haiba nzuri ya mji ndani ya Wilaya ya Kati.
Nae, Asia Abass kwa niaba ya Wananchi wenzake wa Wilaya ya Kati amesema wanaishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Baraza la Mji Kati kwa kuwajengea Bustani za Wananchi, jambo ambalo litawarahisishia huduma hiyo na kuondokana na tatizo la kufuata Viwanja vya kufurahia muda wa mapumziko sehemu za jirani.
Miradi iliyokaguliwa ni Mradi wa Nyumba ya Madaktari uliopo katika Kituo cha Afya Miwani, Mradi wa Vyoo vya Wanafunzi katika Skuli ya Sekondari Ndijani, pamoja na Mradi wa Bustani za Wananchi (Gaden) katika maeneo ya Tunguu na Hanyegwa mchana.