Bodi ya Mkonge kuboresha maisha ya wajasirimali Pemba
26 September 2024, 3:45 pm
Na Mary Julius
Mratibu wa Mradi wa Mkonge na Bidhaa Zitokanazo na Mkonge Zanzibar Joseph Andrew Gasper amesema Bodi ya Mkonge Tanzania ina malengo ya kushirikiana na wajasirimali wa kisiwani Pemba ili kuona wajasiriamali wananufaika na fursa zitokanazo na mkonge.
Akizungumza katika ziara ya kutembelea vikundi 17 vya wajasirimali na wabunifu wa bidhaa za asili kisiwani Pemba, Mratibu Gasper amesema katika kulifanikisha hilo bodi ya mkonge ikishirikiana na Jumuiya ya Nguvukazi Vijana Pemba itaanziasha kituo cha wajasiriamali Pemba ambacho kutakuwa na shughuli mbalimbali za kuwanufaisha wajasiriamali pamoja na kuweza kuvutia wateja.
Amesema kituo hicho kitawasaidia wajasiriamali kutumia bidhaa zinazotokana na mkonge na kujifunza namna gani wanaweza kutumia mkonge katika kujiongezea kipato pamoja na kuwapatia masoko ya bidhaa zao wanazozalisha ili kuimarisha shughuli zao.
Aidha amesema lengo la ziara hiyo ni kuona namna gani wataweza kuboresha maisha ya wajasiriamali kwa kupitia zao la mkonge.
Wakizungumza katika ziara hiyo baadhi ya wajasirimali na wabunifu wa bidhaa za asili wameiomba bodi ya mkonge kutoa msaada wa kimawazo na kimaarifa katika kuwasaidia wajasirimali ili kuweza kuendeleza vitu vya asili.
Aidha wamesema wanahitaji shamba darasa ili kuweza kupata malighafi ya mkonge ambayo itawawezesha kupata malighafi katika mazingira ya eneo la Pemba.