Watembeza wageni Zanzibar wapewa elimu ya homa ya nyani
30 August 2024, 4:58 pm
Na Mary Julius
Wananchi wanaojishughulisha na utoaji wa huduma kwa wageni wanaoingia nchini wametakiwa kuchukua tahadhari katika kujikinga na maradhi ya homa ya nyani ambayo imekuwa ikiripotiwa visa vya wagonjwa katika nchi mbalimbali za jirani na Tanzania.
Akizungumza na wananchi wanaojichughulisha na shughuli ya kupeleka wageni kisiwani Kwale Fumba Afisa Utalii Wilaya ya Magharibi B Hassan Abuu Mohammed na Afisa Maafa Wilaya hiyo Said Chande Said wamesema kila mmoja ana wajibu wa kuchukua tahadhari katika kuhakikisha anajikinga na ugonjwa wa homa ya nyani ambao umekuwa ukiripotiwa katika nchi jirani. Wameeleza kuwa watoa huduma kwa wageni ni miongoni mwa watu wanaopaswa kuchukuwa tahadhari kubwa kutokana na kuwa karibu na watu kutoka mataifa tofauti ambayo yamekuwa yakiripoti wagonjwa , hivyo ofisi ya wilaya imeona ipo haja kuwapatia elimu ya njia sahihi ya kuweza kujikinga .
Akitoa elimu ya kujikinga na homa ya nyani na dalili zake, Afisa Afya Wilaya ya Magharibi B Jabir Suleiman Haji amesema miongoni mwa dalili za homa hiyo ni pamoja na homa kali, uchovu wa mwili, kuumwa na kichwa , kuvimba kwa mitoki ya mwili na malengelenge hasa sehemu za mikono na miguu.
Aidha amewaomba wananchi kujikinga kwa kunawa mikono mara kwa mara kwa maji safi yenye kutiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono, kuepuka kusalimiana pamoja na kuvaa barakoa au kukinga mikono wakati wa kupiga chafya na kuwahi hospitali unapopata dalili hizo.
Baadhi wa wananchi waliopatiwa elimu hiyo ya kujikinga na homa ya nyani wamesema awali walikuwa hawafahamu dalili za maradhi hayo hivyo kupatiwa elimu hiyo kutawawezesha kujikinga na maradhi hayo pamoja na kuwa mabalozi wa kuwaelimisha wengine juu ya kujikinga maradhi hayo.