Jamii Zanzibar yashauriwa kula vyakula vya asili
28 August 2024, 4:53 pm
Na Mary Julius
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Ayoub Muhammed Mahmoud amesema jamii inapaswa kurudi katika zama za nyuma kwa kutumia vyakula vya asili ambavyo vina uwezo wa kuimarisha miili kwa kuwa na afya bora na kutotumia vyakula vya kemikali vinavyosababisha maradhi na kukosa kinga mwilini.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Ayoub Muhammed Mahmoud ameitaka jamii kurudisha utamaduni wa kula zaidi vyakula vya asili kwa lengo la kujenga afya ya mwili na kuepukana na maradhi.
Ameyaeleza hayo huko Makunduchi katika uzinduzi wa Tamasha la vyakula vya asili pamoja na kushiriki zoezi la usafi wa mazingira ikiwa ni shamra shamra za kuelekea siku ya kilele cha tamasha hilo.
Aidha ameisistiza kamati inayoshuhulikia vyakula vya asili na wananchi wa makunduchi kuendelea kuishajihisha jamii juu ya umuhimu ya utumiaji wa vyakula hivyo ili kudumisha mila silka na tamaduni za mzanzibari.
Nae Mratibu wa Tamasha la vyakula vya asili Muhammed Simba Hassan amesema tamasha hilo lina malengo ya kukuza na kuenzi utamaduni pamoja na utalii.
Nao washiriki wa tamasha hilo wamesema ipo haja kwa wananchi wa kijiji hicho kuwaelimisha vijana kuvielewa vyakula vya asili ili kuona vyakula hivyo vinatumika zaidi na kuendelea kutambulikana kwa faida ya vizazi vya sasa na baadae.
Tamasha hilo la siku nne ambalo kilele chake kitafikia tarehe 31 pia litahusisha masuala mbali mbali ikiwemo michezo ya watoto, upimaji wa afya pamoja na ushindani wa upishi wa vyakula vya asili.