Zenj FM

Zanzibar watakiwa kusajili biashara BPRA

25 August 2024, 5:21 pm

Mkurugenzi Mtendaji wa BPRA Khamis Juma Khamis wakati akizungumza na waandishi wa habari Mazizini Mjini Unguja.

Na Thuwaiba Mohammed

Wakala wa Usajili, Biashara na Mali BPRA Zanzibar imesema imeona ipo haja ya kufanya ziara ya utoaji elimu ya uelewa kwa wafanyabiashara na wajasiriamali ambao wanaendesha shughuli zao kiholela bila ya kusajiliwa na taasisi hiyo.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa BPRA Khamis Juma Khamis wakati akizungumza na waandishi wa habari Mazizini Mjini Unguja.

Amesema lengo la kutoa elimu hiyo ni kusaidia wadau, wajasiriamali, wafanyabiashara na wananchi kusajili biashara na mali zao ili kukuza mapato ya taifa na kujua idadi kamili ya wafanyabiashara na wajasiriamali wanaotambulika nchini.

Sauti ya Mkurugenzi Mtendaji wa BPRA Khamis Juma Khamis.

Mkurugenzi Khamis amesema taasisi hiyo inaendelea kutekeleza mikakati yake  ikiwemo kufanya ziara ya utoaji elimu kwa Unguja na Pemba, hivyo amewaomba wananchi, wajasiriamali, wafanyabiashara, taasisi za serikali na zisizo za serikali kujitokeza kwa wingi ili kusaidia taasisi hiyo kutekeleza majukumu yake na kufikia azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Sauti ya Mkurugenzi Mtendaji wa BPRA Khamis Juma Khamis.

Ziara hiyo itajumuisha mikoa yote ya Zanzibar ambapo itaaza mkoa wa Kusini Unguja na kuhitimishwa katika kisiwa cha Pemba.