Ucheleweshwaji wa miradi kero kwa wananchi Pemba
29 July 2024, 5:50 pm
Na Mary Julius
Kumekuwa na ubabaifu wa hali ya juu kwa baadhi ya wakandarasi wanaojenga miradi ya serikali kwa kutotimiza makubaliano ya mikataba jambo ambalo linaisababishia hasara serikali kwa kutofikia malengo ya kuwaletea wananchi maendeleo
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla amesema hajaridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa babara ya Chake-Wete inayojengwa na mkandarasi kampuni ya MECCO iliyotarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi wa nane mwaka huu lakini hadi sasa ujenzi huo bado unasuasua .
Ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara hiyo ambayo kutokukamilika kwake imekuwa ni changamoto kubwa kwa wananchi wanaoitumia barabara hiyo kwa shughuli mbalimbali za kujitafutia kipato.
Makamu wa Pili wa Rais ameitaka kampuni ya MECCO kujitathmini na kufanya uharaka wa kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo ili kurejesha imani kwa wananchi ambao wanapata usumbufu kutokana na uchakavu wa barabara hiyo na endapo watashindwa kukamilisha ujenzi huo kwa wakati uliopangwa watakuwa wamejinyima fursa ya kuendelea kufanya kazi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Akikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa soko la samaki na mbogamboga lililopo Mzambarau Takao na soko la wajasiriamali Kifumbikai Wete Makamu wa Pili wa Rais ametoa mwezi mmoja kwa wananchi waliolipwa fidia kuondoka katika eneo hilo ili kupisha ujenzi wa soko pamoja na kupisha utanuzi wa barabara.
Nao wakandarasi wanaojenga miradi hiyo wamesema ujio wa Makamu wa Pili wa Rais utatatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwa ni pamoja na kucheleweshewa malipo jambo ambalo husababisha kuzorota kwa ujenzi wa miradi hiyo.
Hata hivyo wamemuahidi Makamu wa Pili wa Rais kuwa watafanya kazi kwa jitihada zote ili kuhakikisha wanakamilisha miradi hiyo kwa wakati uliopangwa.