Zenj FM

Ufugaji wa nyuki, nzi fursa kwa wenye ulemavu Zanzibar

18 July 2024, 4:31 pm

Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja Galos Nyimbo akiwa na wajumbe kutoka Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar, katika uzinduzi wa mradi wa kuimarisha uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi kupitia ufugaji wa nyuki na nzi maalum (black soldier flies) kwa watu wenye ulemavu.

Na Mary Julius.

Mradi wa kuimarisha uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi kupitia ufugaji wa nyuki na nzi maalum (black soldier flies) kwa watu wenye ulemavu, umelenga kuimarisha shughuli za utunzaji wa mazingira na kupunguza uvunaji wa bidhaa za misitu.

Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja Galos Nyimbo  amewataka watu wenye ulemavu kuchangamkia fursa za maendeleo zinazopatikana katika mazingira wanayoishi.

DC Nyimbo ametoa wito huo wakati akizindua mradi wa kuimarisha uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi kupitia ufugaji wa nyuki na nzi maalum (black soldier flies) kwa watu wenye ulemavu, uzinduzi uliofanyika katika ukumbi wa mikutano ofisi ya mkuu wa wilaya ya Kusini Unguja. Amesema serikali ya awamu ya nane imeendelea kuwashika mkono  watu wenye ulemavu kwa kuwaletea fursa mbalimbali katika jamii.

Amesema ana imani matokeo ya mradi huo yataongeza ukubwa wa kipato cha watu wenye ulemavu kupitia mauzo ya bidhaa zitokanazo na nyuki sambamba na kuwapatia watu wenye ulemavu uwezo wa kujitegemea na kusimamia shughuli zao.

Aidha Nyimbo amesema wilaya imeupokea mradi huo na  imeshatoa eneo kwa ajili ya kufanyika kwa mradi ili kuweza kuwanufaisha watu wenye ulemavu na jamii kwa ujumla.

Sauti ya Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja Galos Nyimbo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu  Salma Saadat Haji amesema ujio wa maradi huo ni mwendelezo wa kuwawezesha watu wenye ulemavu kiuchumi na kuweza kutunza mazingira kwani mabadiliko ya tabia ya nchi yanawaathiri sana watu wenye ulemavu.

Sauti ya Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu  Salma Saadat Haji.

Naye Mratibu wa mradi huo Mohammed Mohammed amesema mradi umelenga kuwajengea uwezo watu wenye ulemavu katika utunzaji wa mazingira na uimarishaji wa baioanuai kupitia ufugaji wa nyuki  na ufugaji wa nzi maalum (black soldier flies), huku ukitoa fursa endelevu za kujipatia kipato kwa watu wenye ulemavu katika wilaya ya Kusini Unguja  Wilaya ya Kati Unguja na wilaya ya Magharib B.

Aidha amesema mradi huo unatarajiwa kuwanufaisha watu 2000 ambapo wanufaika wa moja kwa moja ni 450 na wanufaika wasio wa moja kwa moja ni 1550.

Nzi Maalum (black soldier flies),
Sauti ya Mratibu wa Mradi huo Mohammed Mohammed.

Akitoa neno la shukrani Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar Asia Abdulsalam Hussein amewaomba maafisa wa serikali, masheha na watu wenye ulemavu kushirikiana kuhamamsisha watu wenye ulemavu kushiriki  katika miradi ya maendeleo.

Sauti ya Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar Asia Abdulsalam Hussein.

Wakizungumza mara baada ya uzinduzi wa maradi huo Mwenyekiti wa Watu Wenye Ulemavu Wilaya ya Kusini Unguja Asha Haji Aweso na Afisa wa Watu Wenye Ulemavu Wilaya ya Kusini Unguja Usi Khamisi Usi wamewataka watu wenye ulemavu kujiunga na mradi ili kukuza kipato pamoja na kutunza mazingira.

Mwenyekiti wa Watu Wenye Ulemavu wilaya ya Kusini Unguja Asha Haji Aweso na Afisa wa Watu Wenye Ulemavu Wilaya ya Kusini Unguja Usi Khamisi Usi.