Zenj FM

Maradhi yasiyoambukiza tishio visiwani Zanzibar

5 July 2024, 3:33 pm

Meneja mradi kutoka Pharm Access Dkt Faiza Abasi katika mkutano wa wadau ulokuwa na Lengo la kujadili mbinu za kumaliza mara maradhi Yasiyoambukiza.

Na Mary Julius.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani WHO, maradhi yanayosababisha vifo vingi zaidi duniani ni ugonjwa wa moyo ambapo watu milioni 17.9 kila mwaka hufariki kutokana na ugonjwa huo, huku ukifuatiwa na saratani watu milioni 9.3 hufariki kila mwaka, ugonjwa wa kisukari ukichukua nafasi ya tatu watu milioni 2.0 hufariki kila mwaka.

Waziri wa Afya Zanzibar Nassro Ahmed Mazrui amesema mapambano ya kumaliza maradhi yasiyoambukiza Zanzibar yanahitaji nguvu ya pamoja na wadau ili kuwa na taifa salama lisilo na maradhi.

Amebainisha hayo katika mkutano wa wadau uliokuwa na lengo la kujadili mbinu za kumaliza maradhi yasiyoambukiza. Amesema mabadiliko ya mtindo wa maisha ndicho chanzo cha magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kutokufanya mazoezi ya kutosha na tabia za uvivu ambayo husababisha kuongezeka kwa uzito wa mwili.

Sauti ya Waziri Wa Afya Zanzibar Nassro Ahmed Mazrui.

Meneja mradi kutoka Pharm Access Dkt. Faiza Abasi amesema maradhi yasiyoambukiza yameathiri watu wengi hapa Zanzibar hali inayopelekea kupoteza nguvu kazi ya jamii.

Dkt. Faiza amesema ni wajibu wa kila mwanajamii kuja na mbinu za kukabiliana na maradhi yasiyoambukiza na siyo kuiachia serikali peke yake katika mapambano haya.

Sauti ya Meneja mradi kutoka Pharm Access Dkt. Faiza Abasi

Kwa upande wake afisa kutoka Kitengo cha Maradhi Yasiyoambukiza Dkt. Lulu Omar Bakar amesema zaidi ya watu elfu tatu wanasumbuliwa na maradhi yasiyoambukiza Zanzibar kwa mujibu wa takwimu za kitengo cha maradhi Yasiyoambukiza Zanzibar

Dkt. Lulu amewataka watu wanaoishi na maradhi yasiyoambukiza kuacha tabia ya matumizi ya tiba za dawa za asili ambazo hazijathibitishwa kitaalam ili kujiepusha na madhara ya dawa hizo.

Sauti ya Afisa kutoka Kitengo cha Maradhi Yasiyoambukiza Dkt. Lulu Omar Bakar

Akiwasilisha mada juu ya maradhi yasioambukiza, Mwenyekiti NCD Alliance Tanzania Prof. Andrew Swai amesema ili tukabiliane na maradhi yasiyoambukiza ni wajibu wa kila mtu kuacha tabia ya kula vyakula vya nafaka vilivyokobolewa pamoja na ukamuaji wa matunda.

Sauti ya Mwenyekiti Ncd Alliance Tanzania Prof.Andrew Swai