Wanawake wahimizwa kuchangamkia fursa za mikopo nafuu
4 July 2024, 5:22 pm
Na Ahmed Abdulla
Wajumbe wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Wanawake Tanzania UWT mkoa wa Kusini Unguja wamehimizwa kuwahamasisha wanawake na vijana kujiunga katika vikundi vya ushirika na kuchukua mikopo nafuu inayotolewa na serikali ili waweze kujiwezesha kiuchumi.
Akizungumza wakati akifungua kikao cha Baraza Kuu la Jumuiya ya Wanawake Tanzania UWT Mkoa wa Kusini Unguja, ukumbi wa Walimu Dunga mjumbe wa Halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa kutoka Mkoa wa Mjini ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza kuu la UWT Taifa, Asya Ali Khamis amesema hatua hiyo itayasaidia makundi hayo kuondokana na mikopo yenye riba kubwa ambayo inarejesha nyuma juhudi zao za kuwaletea maendeleo.
Akizungumzia kuhusu suala la udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto Asya ameitaka jamii kuzingatia umuhimu wa kurejesha utamaduni wa malezi ya pamoja kwa lengo la kupata watoto wenye maadili mema na watakaoweza kulitumikia vyema taifa katika nyanja mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Nae Mwenyekiti wa Umoja Huo mkoani Humo Shemsa Abdalla Ali amewasisitiza wajumbe kuendelea kuulinda mkoa wa Kusini ili ubaki kuwa Ngome ya Chama Cha Mapinduzi.
Nao baadhi ya wajumbe wa baraza hilo wameiomba serikali kuimarisha uharaka wa utoaji wa mikopo kwa akinamama ili kufikia wanawake wengi.
Katika baraza hilo mwakilishi wa viti maalumu mkoa wa Kusini Unguja nafasi za watu wenye ulemavu Mwantatu Khamis Mbaraka amekabidhi kadi 1,500 za jumuiya hiyo kwa wilaya ya Kusini na Wilaya ya Kati.