Zenj FM

Jamii yashauriwa kutumia vituo vya msaada wa kisheria

26 June 2024, 2:54 pm

Jaji wa Mahkama Kuu Zanzibar Jaji Ibrahim Mzee Ibrahim akifungua kongamano la vyuo vikuu la masuala ya msaada wa kisheria, lililofanyika katika Ukumbi wa Aboud Jumbe Tunguu Zanzibar.

Na Mary Julius.

Jaji wa Mahkama Kuu Zanzibar Ibrahim Mzee Ibrahim amewataka wanajamii kuvitumia vituo vya msaada wa kisheria katika maeneo yao ili kupunguza gharama na kufuata huduma hiyo masafa ya mbali.

Akifungua Kongamano la Vyuo Vikuu la masuala ya msaada wa kisheria huko katika Ukumbi wa Aboud Jumbe Tunguu Zanzibar amesema lengo la Serikali kuanzisha vituo hivyo ni kuwaondoshea usumbufu huo na kuitaka jamii kuvitumia ipasavyo ili kufikia malengo yaliokusudiwa.

Amesema msaada wa kisheria ni muhimu sana katika jamii kwani baadhi ya watu hawana uwezo wa kulipia Mawakili hivyo msaada wa kisheria utawajengea ujasiri wa kupambania haki hizo.

Aidha, ameipongeza Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria kuandaa kongamano hilo kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu ambapo litasaidia kuhamasisha upatikanaji wa huduma katika ngazi ya jamii na Vyuo Vikuu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar Hanifa Ramadhan Said amesema madhumuni ya Kongamano hilo ni kuwajengea uzalendo, kujitolea na kuisaidia jamii kupitia msaada wa kisheria.

Aidha amewataka wanafunzi hao kuwaunga mkono katika shughuli mbalimbali zilizoandaliwa na Idara hiyo katika wiki ya msaada wa kisheria hadi kufikia kilele chake Juni 28.

Mapema akitoa salamu za Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP Mratibu na mshauri wa program za utawala bora Godfrey Mulisa amesema Shirika hilo litaendelea kuisaidia Serikali kupitia Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria katika mambo mbalimbali ikiwemo kutoa elimu ya msaada wa kisheria ili Wananchi wapate stahiki zao.

Mratibu na mshauri wa program za utawala bora Godfrey Mulisa akitoa salamu za UNDP katika  kongamano la vyuo vikuu la masuala ya msaada wa kisheria.

Jumla ya mada tatu (3) zilijadiliwa katika kongamano hilo, ikiwemo dhana ya msaada wa kisheria, athari za dawa za kulevya kwa vijana na usafirishaji haramu wa binaadamu na namna ya kuwalinda waathirika ambapo limewashirikisha Wanafunzi kutoka vyuo vikuu mbalimbali vya Zanzibar ikiwemo SUZA, IPA, AL- SUMAIT na ZU.