Zenj FM

Zanzibar Maisha Bora Foundation yasogeza huduma za matibabu Pemba

7 June 2024, 5:15 pm

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib wa pili kutoka kushoto alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari huko Micheweni, kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Mgeni Khatib Yahya.Picha na Is-haka Mohammed.

NA Is-haka Mohammed. Pemba.

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib ametoa wito kwa wananchi wa mkoa wa kaskazini Pemba wenye matatizo mbali mbali na hata wale wasiojihisi kuwa na matatizo kujitokeza kuweza kuchunguzwa afya zao.

Micheweni na Mkoa wa Kaskazini Pemba wanakadiriwa kupatiwa huduma za afya pamoja na kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa mbali mbali katika kambi ya siku tano itakayoanza kesho June 8-12 iliyoandaliwa na Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation iliyo Chini ya Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi.

Akizungumza na waandishi wa habari juu ya kambi hiyo Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib amesema kambi hiyo itajumuisha madaktari bingwa wa magonjwa ya watoto, wanawake na magonjwa mengine mbali mbali.

 Miongoni mwa huduma zitakazopatikana katika kambi hiyo ni pamoja na matibabu ya macho na ugawaji wa miwani, magonjwa ya watoto, akinamama, na uchunguzi wa Saratani ya shingo ya kizazi.

Aidha amesema kuwa uongozi wa serikali ya Mkoa huo pamoja na Wilaya zake mbili umejipanga kuona kila mwananchi anayefika kwenye eneo hilo anapatiwa huduma bora kwa mujibu wa matatizo yake.

Ametoa wito kwa watoa huduma na madaktari wanaoshiriki kwenye kambi hiyo kutoa huduma bora ambazo hazitapelekea malalamiko kwa wananchi watakafika hapo, kwani lengo la taasisi Zanzibar Maisha Bora Foundation ni kuona wananchi wanapatiwa matibabu kutokana na magonjwa waliyoanayo. 

Sauti ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib.

Akizungumza katika Mkutano huo Afisa Mdhamini Wizara ya Afya Pemba Khamis Bilal amesema wizara hiyo imejiandaa vizuri kwa ajili ya kutoa huduma bora za afya ambapo madaktari bingwa wameshawasili kisiwani humo kwa ajili ya kushirikiana na madaktari waliopo Pemba kufanikisha kambi hiyo.

Sauti ya Afisa Mdhamini Wizara ya Afya Pemba Khamis Bilal

Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Mgeni Khatibu Yahya ameushukuru uongozi wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation hasa Mwasisi wake Mama Maria Mwinyi kwa kuipeleka kambi hiyo katika Wilaya ya Micheweni.

Sauti ya Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Mgeni Khatibu Yahya.

Akizungumza kwa Niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Bonaza kutoka Zanzibar Maisha Bora Foundition Ghulam Abdul-karim Ghulam amesema kuanzisha kwa kambi hizo kumelenga kuwasongezea wananchi wa ngazi ya chini kupata huduma za afya.

Kambi hiyo itatanguliwa na bonanza la mazoezi litakalojumuisha vikundi vya mazoezi katika mkoa wa Kaskazini Pemba, ambapo Kambi hiyo inadhaminiwa na Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ)