Waliohusika na ubadhilifu wa mali za umma kufunguliwa mashtaka
2 June 2024, 4:28 pm
Na Mary Julius.
Mwenyekiti wa chama cha Act Wazalendo Na Makamu wa Kwanza wa Rais Othman Masoud amesema viongozi na watendaji wa serikali waliohusika na ubadhilifu wa mali za umma na ufisadi watafunguliwa mashtaka baada ya chama hicho kushika madaraka mwaka 2o25.
Othman ameyasema hayo alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa bububu kwa geji mkoa wa mjini magharib unguja na kudai kuwa ccm inatabia ya viongozi kulindana.
Naye Makamu Wenyekiti wa Chama Hicho Ismail Jussa amesema mradi wa ujenzi wa uwanja wa ndege pemba, barabara za mkoani chakechake, tunguu makunduchi na kisauni fumba umekwama baada ya kiongozi mmoja kuomba rushwa kupitia fedha za mradi huo ambao unaratibiwa na kampuni Parpov na kampuni ya kizalendo ya Mecco.
Akizungumzia ubinafsishaji wa bandari Jussa amesema wawekezaji kutoka ufaransa wameshindwa kuboresha huduma za bandari na badala yake tozo zimeendelea kuongezeka na kuwaumiza wananchi wa Zanzibar.
Chama cha ACT wazalendo kimeanza awamu ya pili ya mihadhara kwa kishindo huku wakitumia muda mwingi kuzungumzia masuala ya demokrasia na utawala bora pamoja na kukosoa vitendo vya ubadhilifu wa mali za umma na ufisadi unaojitokeza katika serikali.